Kampuni ya Taifa Group imetoa tahadhari kwa umma ikionya dhidi ya mpango mkubwa wa utapeli wa uwekezaji unaosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ukitumia jina la ‘TaifaAI’ na utambulisho wa mfanyabiashara, Rostam Azizi.
Kupitia taarifa maalum kwa umma iliyotolewa tarehe 4 Septemba, 2026, kampuni hiyo imeweka wazi kuwa jukwaa hilo linalojiita “TaifaAI” ni la kitapeli na halina uhusiano wowote nao au na Rostam Azizi.
Taifa Group imeeleza kuwa matangazo na maudhui yanayohusu mpango huo yamekuwa yakisambazwa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Instagram yakitumia udanganyifu wa jina, picha, na utambulisho wa Rostam Azizi pamoja na nembo ya Taifa Group ili kuaminisha umma uwepo wa jukwaa la uwekezaji linalotumia teknolojia ya Akili Unde (Artificial Intelligence – AI)
Mpango huo wa kitapeli unalenga kushawishi wananchi kujiunga kwa kuahidi faida kubwa sana za kifedha zisizo za kawaida. Aidha, Taifa Group imefafanua kuwa nukuu na taarifa zote zinazodaiwa kurejea kauli za Bw. Rostam Azizi katika matangazo hayo zimetengenezwa kwa uongo na zina nia ovu ya kupotosha umma
Katika taarifa hiyo, kampuni imetoa mwongozo kwa wananchi ili kujilinda dhidi ya kupoteza rasilimali zao, ikihimiza wananchi kutojiandikisha kabisa katika jukwaa hilo la utapeli, kutotoa taarifa zao binafsi, za kibenki, au za kifedha kwa mtu yeyote, kutotuma wala kuweka fedha zozote kwenye akaunti zinazohusishwa na jukwaa hilo na kuepuka mawasiliano au kufanya miamala na mtu yeyote anayedai kuiwakilisha “TaifaAI” au Taifa Group kuhusiana na mpango huo.
Taifa Group imesisitiza kuwa Rostam Azizi hatumii kamwe jina lake au nafasi yake ya kijamii na kibiashara kuhamasisha wananchi kujiunga na miradi ya uwekezaji mtandaoni, mifumo ya biashara ya kidijitali, au mipango yoyote inayowaahidi wananchi kupata faida za haraka za kifedha
“Taifa Group inachukua hatua stahiki kutoa taarifa kuhusu maudhui haya ya kitapeli kwa mamlaka husika pamoja na watoa huduma wa majukwaa ambako maudhui hayo yanasambazwa. Tunawasihi wananchi kuwa waangalifu na kusambaza tahadhari hii kwa wengine, hususan kwa mtu yeyote ambaye amepokea au kuona tangazo hili la kitapeli. Taifa Group haitawajibika kwa hasara yoyote itakayotokana na mtu kujihusisha na mpango huu wa kitapeli”, imeeleza taarifa hiyo.
Kwa taarifa rasmi kuhusu Taifa Group na shughuli zake, wananchi wameshauriwa kutegemea taarifa zinazotolewa kupitia njia rasmi za mawasiliano za Taifa Group pekee.