SHIRIKA lisilo la kiserikali la Inades Formation Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa punda wamekutana katika Kata ya Migoli, halmashauri ya Wilaya ya Iringa, kujadili masuala ya haki na ustawi wa mnyama punda, ambaye ni sehemu muhimu ya shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa eneo hilo.
Akizungumza katika kikao hicho, Afisa Mifugo wa Kata ya Migoli, Charles Koti, amesema uwepo wa Jukwaa la Mnyama Kazi Punda unalenga kuhakikisha punda wanapata haki na huduma stahiki, ikiwemo kulindwa dhidi ya mateso na majeraha, kupata makazi salama, chakula cha kutosha, matibabu pamoja na muda wa kupumzika.
Koti amesema licha ya wananchi wengi kuwa na uelewa kuhusu haki hizo, bado utekelezaji wake haujawa wa kuridhisha, hali inayodhihirishwa na kuwepo kwa punda wanaotumika katika shughuli mbalimbali wakiwa na majeraha na wakati mwingine katika mazingira yasiyofaa.

Kwa upande wake, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa Inades Formation Tanzania, John Militon, amesema elimu iliyotolewa kwa walengwa katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi imekuwa na manufaa makubwa, kwa kuwa sehemu kubwa ya wakazi wa Migoli hutegemea punda katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Militon amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna umuhimu wa kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa elimu kuhusu utunzaji na ustawi wa punda, ili kuhakikisha mnyama huyo anatumika kwa tija bila kukiukwa kwa haki zake.
Naye Afisa Kiungo wa Mradi wa Inades Formation Tanzania, Iringa DC, Isdory Karia, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa mafunzo shirikishi kwa wananchi na wadau, akipendekeza mpango wa elimu kuhusu ustawi wa punda uendelezwe katika ngazi za serikali za kata, tarafa hadi wilaya.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Mnyama Kazi Punda Kata ya Migoli, Spelansia Kinyaga, amesema elimu iliyotolewa imeanza kuleta mabadiliko chanya katika jamii, ambapo baadhi ya wananchi wameanza kufuga punda na kuwakodisha kwa ajili ya shughuli mbalimbali, hatua inayowawezesha kujipatia kipato na kuboresha maisha yao.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Jukwaa hilo ambaye pia ni Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Jesca Makalwe, amesema ni muhimu kuwepo kwa sheria ndogondogo zitakazowaongoza wananchi na viongozi katika kuhakikisha haki na ustawi wa punda vinalindwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria hizo ili kuzuia vitendo vya ukatili na uvunjwaji wa haki za mnyama huyo.

