Leo Septemba 3, 2026, katika mwendelezo wa kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, shahidi wa tatu ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Amani Golugwa, ameendelea kutoa utetezi wake mahakamani hapo huku akiongozwa na Lissu katika kutoa ushahidi huo.
Katika ushahidi wake, Golugwa ameanza kwa kuwasilisha mbele ya majaji tathmini na kauli zilizotolewa na watazamaji wa uchaguzi wa mwaka 2025 kutoka mataifa mbalimbali na jumuiya za kimataifa na kikanda.
Ameeleza kuwa taarifa ya watazamaji wa uchaguzi kutoka SADC ilihitimisha kuwa uchaguzi wa Tanzania ulishindwa kukidhi vigezo vya viwango vya kidemokrasia, ulikuwa na vitisho kwa viongozi wa upinzani, ukakosa ushindani sawa na uwazi, na ulikumbwa na udanganyifu pamoja na vurugu siku ya uchaguzi, jambo lililoufanya kukosa uhalali wa kuitwa uchaguzi.
Shahidi huyo ameendelea kueleza kuwa watazamaji wa uchaguzi wa Jumuiya ya Ulaya (EU) nao walionesha kusikitishwa na matukio ya vurugu, uharibifu wa mali, kuzimwa kwa mitandao ya mawasiliano, na ripoti za mauaji yaliyotokea kabla na wakati wa uchaguzi, wakiwemo watu waliotekwa, kupotezwa na kuuawa, wakihitimisha kuwa uchaguzi huo haukuwa huru wala wa wazi.
Kuhusu Jumuiya ya Madola, Golugwa ameeleza kuwa alimsikia Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo akisikitishwa na kuhuzunishwa na vurugu na mauaji yaliyotokea, akiahidi kuwa jumuiya hiyo ingefuatilia tukio hilo kwa karibu.
Akigusia msimamo wa Thabo Mbeki Foundation, Golugwa ameeleza mahakama kuwa taasisi hiyo ilieleza mambo manne makubwa, yakiwemo kwamba uchaguzi wa Tanzania ulikuwa chini ya miongozo ya kidemokrasia ya SADC na Umoja wa Afrika, wapiga kura walikosa uhuru wa kutimiza wajibu wao kutokana na vurugu, matokeo ya urais na ubunge hayakuwa ya kweli wala ya halisi na utashi wa wananchi, na kwamba nchi haikuwa na serikali yenye uhalali bali serikali hiyo iliwekwa kwa mabavu kupitia uchaguzi batili.
Ameongeza kuwa waangalizi walibainisha vyombo vya dola, hususan polisi, viliwapiga waandamanaji na kuwazuia au kuwanyanyasa waangalizi, huku akimnukuu Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman aliyeripoti kuwa watu 518 waliuawa wakati wa uchaguzi mkuu huo.
Kuhusu kesi yenyewe inayomkabili Lissu, Golugwa ameeleza kuwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lilieleza kukamatwa kwa kiongozi huyo kuwa si halali, kunakominya uhuru wa kujieleza na kwamba shtaka hilo ni katili lenye lengo la kumuumiza kisiasa.
Ameongeza kuwa kikao cha mawaziri wa Jumuiya ya Madola (CMAG) nacho kilithibitisha kuwa kesi hiyo inadhihirisha uminywaji wa demokrasia, ni batili, na kutaka Lissu aachiliwe huru bila masharti. Akijibu maswali kuhusu mfumo wa usimamizi wa uchaguzi, Golugwa ameeleza mahakamani hapo kuwa Tume Huru ya Uchaguzi, kuanzia Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, wajumbe, Mkurugenzi wa Uchaguzi, hadi wasimamizi wa majimbo na vituo ambao ni watumishi wa umma katika ngazi za kata, mitaa, na vijiji, wote huteuliwa moja kwa moja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hali inayofanya mfumo mzima kukosa uwazi.
Kuhusu mkutano uliofanyika tarehe 3 Aprili 2025, shahidi huyo amefafanua kuwa uliandaliwa na sekretarieti ya chama kwa wazo la Katibu Mkuu kwa ajili ya watia nia waliotaka kugombea, huku ukihudhuriwa pia na viongozi wa kanda, mkoa, jimbo na viongozi wakuu wa kitaifa wakiwemo Mwenyekiti, Makamu Wenyeviti wa Bara na Zanzibar, na Makatibu Wakuu.
Amekanusha vikali madai kuwa Tundu Lissu ndiye aliyeitisha mkutano huo, akieleza kuwa yeye alifanya mawasiliano kwa simu na viongozi wakuu ili kuwaita wahusika wa mkutano huo, na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia, akiwaita waandishi wa habari. Amesema kwamba Tundu Lissu hakuwepo bali alikuwa kwenye ziara ya operesheni ya chama ya “No Reforms No Election” katika Kanda ya Nyasa iliyojumuisha mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, na Songwe.
Golugwa amesisitiza kuwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kama Clouds TV, Jambo Online TV, The Chanzo Online TV, ITV, na gazeti la Mwananchi walialikwa na Brenda Rupia bila kuwekewa masharti yoyote, na kwamba hapakuwa na maelekezo yoyote yaliyotolewa na Lissu kwa vyombo vya habari.
Amefafanua kuwa matangazo ya moja kwa moja yaliyofanywa na Jambo TV na The Chanzo yalikuwa chini ya umiliki na mamlaka ya vyombo hivyo vyenyewe vya habari, akitupilia mbali madai kuwa Lissu ndiye aliyefanya matangazo hayo au kuchapisha maneno yaliyodaiwa kuwa ni ya kiuchochezi kwenye mitandao ya Jambo TV.
Akihitimisha ufafanuzi kuhusu maneno yaliyosomewa mahakamani ikiwemo kauli ya “msimamo huu unaashiria uasi”, “tutauvuruga uchaguzi”, na “tunaenda kukinukisha vibaya sana”, Golugwa ameeleza kuwa maneno hayo hayakumtaja hata mara moja Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Baraza la Mawaziri, Mwanasheria Mkuu, Mkurugenzi wa Mashtaka, wala vyombo vya ulinzi na usalama kama Jeshi la Polisi, JWTZ, Mgambo, Usalama wa Taifa, au Jeshi la Magereza, na kwamba neno “Serikali” halikuwepo.
Amesisitiza kuwa kwa ufahamu wake, kusema “kukinukisha” ni neno la kisiasa lenye ujasiri linalomaanisha kusababisha harufu itoke au kuwa na msimamo thabiti, na kisheria nchini Tanzania matamshi hayo, pamoja na kupinga mifumo ya uchaguzi au kusema uasi, hayafikii kiwango cha kutenda kosa la uhaini au uhalifu wowote.
Baada ya utetezi wake kufikia hapo, Wakili wa serikali alisisimama na kuwaomba Majaji kuahirisha kesi kwa muda ili kuruhusu mapumziko. Majaji walikubali ombi hilo na kuahirisha shauri hilo kwa muda wa saa moja na nusu huku likitarajiwa kuendelea tena saa nane na nusu mcha wa Septemba 3, 2026