MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umekutana na wajumbe wa kamati za vijiji, mazingira, maliasili, jumuiya za watumiaji maji, majanga pamoja na maafa kutoka wilaya tano, katika semina fupi iliyolenga kutathmini ushiriki wa makundi yote katika jamii.
Semina hiyo imewakutanisha wajumbe kutoka wilaya za Mufindi, Kilolo, Wang’ing’ombe, Mbalali na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ikiwa ni sehemu ya tathmini ya awali baada ya ukaguzi uliofanywa kupitia kamati hizo.

Akizungumza mara baada ya semina hiyo, mwezeshaji Wilfred Kurwa amesema washiriki wameweza kubaini changamoto mbalimbali zinazokwamisha ushirikishwaji wa makundi yote, ikiwemo ushiriki mdogo wa wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi.
Amesema pia kundi maalumu, wakiwemo watu wenye ulemavu, bado halijashirikishwa kikamilifu katika baadhi ya kamati, hali inayohitaji hatua za pamoja ili kuhakikisha kila kundi linapata nafasi ya kutoa mchango wake katika maendeleo ya jamii.
Kurwa ameongeza kuwa TGNP inapanga kuandaa mpango kazi shirikishi utakaojumuisha makundi yote katika jamii, wakiwemo watu wenye ulemavu na vijana, ili kuongeza ushiriki wao katika uongozi na kufanya maamuzi.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema semina hiyo imewajengea uwezo na kuwakumbusha umuhimu wa kuwashirikisha wanawake na makundi mengine katika nafasi za uongozi na maamuzi, wakisisitiza kuwa makundi hayo yana mchango mkubwa katika maendeleo yanapopewa nafasi.
Wamesema baada ya kurejea katika maeneo yao, watakuwa mabalozi wazuri kwa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa ushirikishwaji wa makundi yote, kwa lengo la kujenga jamii yenye usawa na inayotoa fursa kwa kila mmoja kushiriki katika maamuzi na maendeleo.
