Latest Posts

PROF. KABUDI: ZINGATIENI TAHADHARI ZINAZOTOLEWA NA WATAALAMU DHIDI YA MAJANGA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amewataka wananchi kuzingatia kwa umakini tahadhari na maelekezo yanayotolewa na wataalamu pamoja na mamlaka husika ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na majanga na maafa.

Prof. Kabudi ametoa wito huo Agosti 19, 2026, wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Watoa Huduma za Misaada ya Kibinadamu Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo amesisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi ni nguzo kuu katika kuimarisha ustahimilivu wa jamii.

Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema ili kuongeza uwezo wa nchi katika kukabiliana na maafa kwa ufanisi, huku akibainisha kuwa kufanikisha hilo kunategemea mifumo madhubuti na uratibu wa karibu kati ya Serikali na wadau wa huduma za kibinadamu.

Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake uliotukuka katika kusimamia masuala ya kibinadamu na kuhakikisha wananchi wanaokumbwa na dharura wanapata msaada na faraja kwa wakati.

Pamoja na pongezi hizo, amewataka watoa huduma za kibinadamu kuwekeza zaidi katika kutoa elimu na taarifa sahihi kwa wananchi kuhusu vihatarishi vilivyowazunguka, pamoja na hatua zinazopaswa kuchukuliwa kabla, wakati, na baada ya janga kutokea.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. James Kilabuko, amebainisha kuwa maadhimisho hayo yanatoa fursa ya kutambua na kuthamini mchango wa watoa huduma za kibinadamu wanaojitolea kwa ujasiri na huruma kuokoa maisha ya watu.

Dkt. Kilabuko amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano huo ili msaada uweze kuwafikia walengwa kwa wakati, huku akiongeza kuwa katika kila hatua ya utoaji huduma, utu, usalama, na maisha ya mwanadamu lazima viwe kiini cha maamuzi yanayochukuliwa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!