Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imeingia katika ushirikiano wa kimkakati na taasisi ya ELLA Foundation, wenye lengo la kuwawezesha watu wenye changamoto ya usikivu (uziwi) kupitia mafunzo ya ujuzi na kuwatafutia soko la bidhaa zao kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.
Katika kuitafsiri dhana ya utekelezaji wa wajibu wa taasisi kwa jamii (CSR), TISEZA itaanza kununua mifuko yenye ubunifu wa hali ya juu inayotengenezwa na wanufaika wenye uziwi na kuitumia kama sehemu ya vifaa rasmi na zawadi kwa wawekezaji na wadau mbalimbali wanaokuja nchini. Hatua hii inalenga kuwapa vijana hao soko endelevu na kuonesha uwezo wa Watanzania wenye mahitaji maalum katika kuzalisha bidhaa bora.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam katika hafla ya utiaji saini na makabidhiano ya awali leo Agosti 19, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, amesema ushirikiano huo ni sehemu ya dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuleta uchumi jumuishi.
“Tumekuwa na taratibu ya kutumia bidhaa za Kitanzania zikiwa sehemu ya kuonesha uwezekaji unaofanyika Tanzania… Lakini sasa pia tutaongeza bidhaa hizi ambazo zimetengenezwa na wadau ambao ni wa kwenye makundi maalum. Hatua hii itawasaidia kuwapatia wanufaika soko endelevu la bidhaa zao na kuongeza fursa za kiuchumi kwa watu wenye makundi maalum,” amebainisha Teri.

Kwa upande wake, Muasisi wa ELLA Foundation, Esther Jaswant ameeleza kuwa ushirikiano huo unatuma ujumbe mzito kwa jamii na wawekezaji kuwa ulemavu si kizuizi cha tija katika uchumi
“Mtu ambaye ana ulemavu hiyo sio kikwazo chake kupata fursa na pia kupata kujikimu kimaisha ama kupata uhuru wa kiuchumi. Mojawapo ya miradi yetu mikubwa ni ELLA workshop ambapo tunazalisha bidhaa zenye ubora… na kuwasaidia hawa viziwi kushiriki kwenye uchumi na kujitegemea kifedha,” amesema Jaswant.

Ushirikiano huu unatarajiwa kuwa wa muda mrefu, ambapo TISEZA imejipanga pia kuwashawishi wawekezaji wanaokuja nchini kutoa kipaumbele cha ajira kwa watu wenye ulemavu katika viwanda vyao, ikizingatiwa kuwa kazi nyingi za viwandani ni zile zinazoweza kufundishika kwa urahisi

Hadi sasa, karakana ya ELLA Foundation inahudumia vijana 10 ambao wamebobea katika ufundi na ujuzi wa ubunifu.
