Leo Agosti 13, 2026, Raia wa Zambia wanapiga kura kuchagua viongozi wengine wapya watakao liongoza taifa hilo. Uchaguzi huo unamuhusisha Rais wa sasa Hakainde Hichilema na upinzani unaotafuta mabadiliko ya kiuongozi nchini humo.
Hichilema, mwenye umri wa miaka 64, anawania muhula wa pili akijinadi kwa ahadi za ajira na kufufua uchumi wa taifa hilo.
Zambia inajulikana kwa demokrasia imara Afrika ingawa hivi karibuni uongozi wa sasa umekuwa ukikosolewa kwa madai ya kubana wapinzani na kuminya uhuru wa kutoa maoni, hali iliyoibua wasiwasi wa kisiasa nchini humo.
Mpinzani mkuu kati ya wagombea 13 ni Brian Mundubile ambaye ni Waziri wa zamani wa utawala wa Edgar Lungu. Mundubile ameahidi maridhiano na mabadiliko ya kitaifa.
Mundubile anaongoza Chama kipya cha NRPUP chenye uungwaji mkono mkubwa wa upinzani. Uchaguzi huo unatajwa kuwa na ushindani mkali huku wengi wakisubiri kuona matokeo yake.