Latest Posts

“LEO WATOTO WANGU WALALE KWA AMANI”, LISSU AKIWASILISHA HOJA ZAKE ZA MWISHO

Katika kuendelea kuwasilisha hoja zake za mwisho, Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, amezungumzia hoja ya nne kati ya 9 ambazo alizotaja jana Septemba 23, 2026 kama sehemu ya hoja zinazodaiwa na jamhuri kuwa ushahidi wao katika kesi hiyo.

Eneo hilo la nne linahusu “Maneno yaliyotamkwa na mshtakiwa, yanatengeneza kosa lolote linalojulikana na Sheria?, ambapo Tund Lissu amefafanua kwa kuanza kurejea maneno hayo ambayo yalitumika kama kielelezo cha kufungua kesi hiyo ya uhaini yanayodaiwa kutolewa katika mkutano uliofanyika Aprili 3, 2025.

Maneno yenyewe yanasema hivi, nitayanukuu;

“Wanasema kitu kimoja sahihi hapa, wanasema hivi msimamo huu unaashiria uasi. Ni kweli, ni kweli kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi na hiyo ndiyo namna ya kupata mabadiliko kwa hiyo tunaenda kukinukisha sana sana. Huu uchaguzi tutauvuruga, tutauvuruga kwa sababu tunaenda kuuvuruga sana sana.”

Kuhusu maneno yake, Lissu amesema kwamba hakuna mahali popote ambapo upande wa mashtaka umeyafafanua maneno hayo. Amesema hawajasema “kuvuruga uchaguzi” maana yake ni nini na kwa nini ni kosa. Amesema hawajasema “kuhamasisha uasi” ni nini na kwa nini ni kosa, pia amesema hawajasema “kuzuia uchaguzi” ni nini na kwa nini ni kosa, hawajafafanua “kukinukisha” ni nini na kwa nini ni kosa, na kuwa si wajibu wake kama mshtakiwa kuyatolea maneno hayo ufafanuzi.

Lissu amesema kuwa mashahidi wote wa upande wa utetezi wamesema maneno ya Lissu hayana shida na si kosa kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akieleza kwamba uhaini ni ule unaofafanuliwa na sheria na nje ya hapo ni maneno matupu.

Lissu amesema kuwa yapo maeneo kumi kulingana na sheria ambayo yanaweza kutengeneza kosa la uhaini. Ameyataja maeneo hayo au vitendo hivyo akieleza kuwa kitendo cha kwanza kilichoelezewa kwenye kifungu cha 39 ni pamoja na:

  1. Kumuua au kujaribu kumuua Rais.
  2. Kuendesha vita dhidi ya Jamhuri ya Muungano.
  3. Kutengeneza nia ya kuwezesha au kuhamasisha mtu au kikundi cha watu wasababishe kifo cha watu au Rais atiwe kilema au ajeruhiwe.
  4. Kitendo cha nne ni kutengeneza nia ya kuwezesha au ukatengeneza nia ya wengine wawezeshe Rais apinduliwe kwa njia zisizo halali kutoka kwenye nafasi yake kama rais na jina lake kama mkuu wa nchi na amiri jeshi mkuu ni kitendo cha uhaini 39(2)(b)
  5. Kutengeneza nia ya kuwezesha au kuchochea mtu au kikundi cha watu waweze kuipindua kwa njia zisizo halali Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
  6. Kutengeneza nia au kuwezesha au kuchochea wengine kuwezesha kutishiwa kwa Serikali, Bunge, au Mahakama ya Jamhuri ya Muungano.
  7. Kujiunga au kujishirikisha na maadui wa Jamhuri ya Muungano au kuwapa msaada, vinywaji, chakula, au malazi.
  8. Kuchochea mtu yeyote ndani au nje ya Jamhuri ya Muungano kuivamia kwa silaha.
  9. Kuchukua silaha ndani ya Jamhuri ya Muungano kwa lengo la kuilazimisha kubadili uelekeo.
  10. Kusaidia maadui wa Jamhuri ya Muungano kwa kufanya kitendo chochote ambacho kina lengo la kuathiri usalama au kuzuia Serikali ya Jamhuri ya Muungano au operesheni za kijeshi au za polisi.

Lissu amesema kuwa nje ya makosa hayo kumi ambayo ameyataja kwa kurejea Kanuni ya Adhabu, Kifungu cha 39 maneno yaliyotumika kumshtaki ni ya hisia.

*Tuanze na neno tutavuruga uchaguzi, liko wapi kwenye hiyo list ya matendo 10 ya kihaini? Kuzuia uchaguzi, iko wapi?, kuhamasisha uasi kwa kingereza ni rebellion iko wapi kwenye Section 39??? Iko wapi Waheshimiwa majaji ili nilale usingizi mzuri leo kuwa nilisema maneno yanayokiuka sheria, ni wapi?? haipo. Kukinukisha, iwe kukinukisha vibaya sana, kukinukisha sana sana ili angalua leo wanangu wherever they are walale kwa amani kuwa baba yao aliongea maneno ambayo yanakiuka sheria, yako wapi?? Hayapo waheshimiwa majaji.” amesema Lissu

Lissu amesema kuwa yale ambayo yametajwa kwenye sheria kama uhaini hayahusiani kabisa na maneno ambayo yeye aliyatamka Aprili 3, 2025, akisisitiza kuwa amefungwa bure na ameonewa.

Amesema kwamba ninamnukuu “Waheshimiwa majaji, nimefungwa bure, nimeonewa; jela mwaka mmoja na nusu. Nina ndugu, nina wanachama hapa wanatoka nchi nzima. Mwenyekiti wao amefungwa mwaka na nusu, nipo gerezani nalindwa na askari sijui utafikiri muuaji wa aina gani,” amesema Lissu

Ameongeza kwamba Ushahidi wote unahusu uchaguzi na mashahidi wote wanazungumzia uchaguzi. Akirejea Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, sura ya saba ambayo imeorodhesha makosa 23 na adhabu zake kuanzia kifungu cha 114 hadi 136, ambapo amesema kuwa aliyataja ili kuionesha mahakama kama katika makosa yaliyotajwa lipo kosa linalotokana na maneno yake.

Amesema kuwa hakuna sehemu inayosema kuzuia uchaguzi sio kosa, kuhamasisha watu kuzuia uchaguzi sio kosa, kukinukisha sio kosa, au kufanya uasi dhidi ya uchaguzi sio kosa, kwani kifungu cha tano cha Kanuni ya Adhabu kimefafanua kuwa kosa ni kitendo, jaribio, au kufanya kitu ambacho sheria imekiwekea adhabu.

Lissu amesema makosa yanayodaiwa ya kihaini sio uhaini kwa mujibu wa Kifungu cha 39 cha Kanuni ya Adhabu, na sio makosa kwa mujibu wa makosa yaliyoorodheshwa na Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024.

Jambo la tano lilihusu kwamba, Je kutamka yale maneno yanayolalamikiwa ni kitendo? kwa mujibu wa Kanuni ya Adhabu kifungu cha 39(2)(d) akihoji kwamba, Je maneno ni matendo?

Lussu ameeleza kwamba, mkanganyiko huo umetengenezwa kwa makusudi na upande wa mashtaka na kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 39(2)(d) ambacho amesema Masharti ya hicho ni kufungu ni kuwa lazima uthibitishe nia ya kutenda kosa la uhaini kwa kuchapisha au kutenda kitendo cha wazi kuwa kosa alilofanya ni kusema maneno na akirejea kesi ya Khatibu Ghandi ni kuwa maneno matupu hayatengenezi uhaini.

Amesema hati ya mashtaka ilitengenezwa kwa kusema mshtakiwa alidhihirisha nia kwa kitendo chake cha kutamka wakitafuta namna ya kuhalalisha kusema maneno ya Lissu kuwa ni vitendo.

Anasema kwa mujibu wa kamusi ya Oxford Advanced Leaners Dictionary ‘Act’ ni kitu ambacho mtu anakifanya. Deed, kwa mujibu wa kamusi ya Oxford Advanced Leaners Dictionary ni kitu ambacho mtu anakifanya na yana maana sawa na neno Act.

Amesema kwamba Kwa mujibu wa kamusi ya kisheria ya Black’s Law Dictionary toleo la saba inasema ‘Act’ ni kitu ambacho kimefanywa na ina maana sawa na neno ‘deed’ .

Amesema kuwa maneno hayawezi yakawa matendo na hati ya mashtaka inayosema alithibitisha nia ya kufanya uhaini kwa maneno yake ya matendo ni ‘nonsense’ ni kitu hakiwezekani kwa sababu mabeji hayawezi kuwa matendo na kwa mujibu huo hati ya mashtaka amesema ni mbovu.

Lissu amewashukuru wanaomsaidia akisema “Mawakili wanaonisadia wanafanya kazi kubwa sana na Mungu awasaidie”

Lissu amesema kwamba, vyovyote ambavyo majaji wataamua watatengeneza msingi kwa miaka ijayo na kutoa msimamo juu ya maneno hayo mawili, akisema hii ni sehemu moja ambapo busara zao zinahitajika katika kutoa mwongozo kwa ajili ya baadaye, akitumia neno “future'”.

Amesema kuwa jibu la swali lake la tano ni kuwa hasi ikimaanisha kwamba ‘deed'(kitendo) sio sawa na maneno yaliyotamkwa. Amesema hati ya mashtaka haitibiki, ni mbovu kwa namna ambayo haitibiki akisema wameingiza maneno ambayo si maneno ya kisheria. Lissu amesema.

“Maneno yanayoeleweka mtaani yanaingizwa kwenye nyaraka za kisheria kwenye hati ya mashtaka”

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!