Wananchi wa Kata ya Mwabuzo, Wilaya ya Meatu, Mkoa wa Simiyu, wamepongewa kwa juhudi zao za kuchangisha fedha na kujenga Kituo cha Polisi katika kata hiyo, hatua inayoonesha ushirikiano na imani waliyonayo kwa Jeshi la Polisi katika kulinda amani na usalama wa jamii.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Christina Musyani kutoka Kamisheni ya Polisi Jamii, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, ametoa pongezi hizo leo Septemba 26, 2026, baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa Polisi Kata katika Kata ya Mwabuzo.
SACP Musyani amepongeza wananchi hao kwa kuchukua hatua ya kujenga kituo hicho kwa nguvu zao, akieleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya ushirikiano mzuri kati ya wananchi na Jeshi la Polisi katika kuhakikisha wanakuwa na huduma za Polisi zilizo karibu na jamii.

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu na changamoto nyingine za kiusalama, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wakati.
Ujenzi wa Kituo hicho cha Polisi umefanywa kwa nguvu za wananchi wa Kata ya Mwabuzo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za wananchi kuhakikisha wanapata huduma za Polisi kwa urahisi na kuimarisha ulinzi na usalama katika eneo lao.
