Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetangaza rasmi kutotambua mchakato na matandazo ya mabadiliko ya jezi za timu za taifa yaliyofanyika bila kuishirikisha wizara hiyo, licha ya kuwepo kwa maelekezo yaliyotolewa tangu mwezi Februari 2026.
Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda, ambaye amesema kuwa Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi katika maandalizi ya timu za taifa zinazoshiriki mashindano ya kimataifa, ikiwa ni maandalizi muhimu kuelekea Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.

Waziri Makonda amefafanua kuwa uwepo wa michuano hiyo mikubwa nchini unatoa fursa ya kuboresha muonekano wa jezi za timu za taifa ili ziakisi utambulisho wa nchi na kulinda manufaa mapana ya taifa badala ya maslahi binafsi.
Kufuatia hali hiyo, Waziri ametangaza kuunda Kamati maalum ya kuchunguza mkataba wa mzabuni aliyetengeneza jezi hizo, kwa lengo la kubaini uhalali wake, faida inayopatikana kwa timu za taifa, na namna mauzo ya jezi hizo yanavyoweza kuchangia katika kuendesha timu hizo badala ya kuwa mzigo kwa Serikali pekee.
Taarifa hiyo imehitimishwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Zaituni Mkwama, kwa niaba ya Wizara hiyo, ikisisitiza msimamo wa Serikali wa kusimamia maslahi ya michezo nchini.