Latest Posts

TANZANIA YATUMIA JUKWAA LA KOREA KUVUTIA UFADHILI WA MIRADI YA KIMKAKATI YA MAJI

Tanzania imeendelea kutumia fursa za majukwaa ya kimataifa kuimarisha ushirikiano na washirika wa maendeleo, ikiwemo Serikali ya Korea Kusini, katika kutafuta uwekezaji na ufadhili wa miradi ya kimkakati ya maji nchini.

Katika hatua hiyo, Tanzania imeiomba Serikali ya Korea Kusini kuongeza ushirikiano na uwekezaji katika sekta ya maji, hususan katika ujenzi wa mabwawa, uendelezaji wa Gridi ya Taifa ya Maji na uanzishaji wa mifumo ya kisasa ya usimamizi wa huduma za maji.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, wakati wa mazungumzo yake na Naibu Waziri wa Tabianchi, Nishati na Mazingira wa Korea Kusini, Kum Hanseung, yaliyofanyika Septemba 9, 2026, jijini Daegu, pembezoni mwa Kongamano la Kimataifa la Maji la Korea (Korea International Water Week 2026).

Mhandisi Kundo amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Korea Kusini umeendelea kuimarika kwa zaidi ya miaka 30, ambapo Sekta ya Maji imekuwa miongoni mwa sekta zinazonufaika kwa kiasi kikubwa na ufadhili wa Korea Kusini kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi (Economic Development Cooperation Fund – EDCF).

Amesema kati ya dola za Marekani milioni 660 zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea nchini, dola milioni 248.3 zimeelekezwa katika Sekta ya Maji, hatua inayoonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora na endelevu za maji.

“Tanzania inalenga kupanua zaidi ushirikiano huu kwa kushirikisha taasisi mbalimbali za Korea Kusini katika kuandaa na kufadhili miradi ya kimkakati ya maji yenye tija kwa wananchi na maendeleo ya Taifa,” amesema Mhandisi Kundo.

Ameeleza kuwa Tanzania inatarajia kushirikiana zaidi na taasisi za Korea Kusini, zikiwemo Korea EXIM Bank, K-Water, KOICA na Korea Water Forum, katika maeneo ya usalama wa maji, mifumo ya tahadhari za mapema dhidi ya majanga yanayohusiana na maji, matumizi ya teknolojia za kisasa za kupunguza upotevu wa maji, pamoja na utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya maji na usafi wa mazingira katika vijiji 1,575.

Aidha, Mhandisi Kundo amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Korea Kusini tayari umezaa matokeo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji nchini, ikiwemo mfumo wa Usimamizi Mahiri wa Maji (Smart Water Management) unaotekelezwa katika Mamlaka ya Maji Iringa, pamoja na miradi ya kutibu maji taka katika miji ya Dar es Salaam, Iringa na Dodoma.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Tabianchi, Nishati na Mazingira wa Korea Kusini, Kum Hanseung, ameeleza utayari wa nchi hiyo kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha sekta ya maji, hususan katika matumizi ya teknolojia, ubunifu na uendelezaji wa miradi inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za maji na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Akihitimisha mazungumzo hayo, Mhandisi Kundo amesisitiza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kuandaa, kutekeleza na kufadhili miradi ya kimkakati ya maji kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na endelevu.

Aidha, Mhandisi Kundo amemkaribisha Naibu Waziri Hanseung kushiriki katika Wiki ya Maji Tanzania, itakayofanyika kuanzia tarehe 16 hadi 22 Machi 2027, nchini Tanzania, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza majadiliano, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika sekta ya maji.

Katika ziara hiyo, Mhe. Kundo ameambatana na Mhe. Anna Richard Lupembe na Mhe. Ramadhani Hamza Singano, ambao ni Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Maji na baadhi ya taasisi zake.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!