Latest Posts

“MASILAHI YA CHAMA SI BINAFSI”, MNYIKA ACHARUKA BAADA YA UPANDE WA JAMHURI KUMTAJA KAMA SHAHIDI WA MASILAHI

Baada ya mapumziko mafupi mchana wa leo, kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Antiphas Lissu, ilirejea huku Katibu Mkuu wa chama hicho, John John Mnyika, akipanda kizimbani kukabiliana na maswali ya dodoso kutoka kwa Wakili wa Serikali Mkuu, Nassor Katuga.

Moja ya maeneo yaliyozua mjadala ni pale Katuga alipohoji kama raia yeyote, ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa CHADEMA, ana haki ya kuzuia uchaguzi mkuu uliowekwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Mnyika alitoa jibu akisema, “Ni haki kwa uchaguzi usio huru na wa haki, ni haki kuuzuia kwa njia za kidemokrasia. Ni haki kabisa”. Amesisitiza kuwa wananchi wana haki ya kushiriki uchaguzi ukiwa huru, wa haki na halali tu.

Katuga alimtaka Mnyika kufafanua kile alichokisikia wakati wa hotuba ya Tundu Lissu katika mkutano wa watia nia wa Aprili 3, 2025. Mnyika alikiri kusikia kauli za ‘Polisi kukimbia na mabegi ya kura’, ‘tunaenda kuzuia uchaguzi’ na ‘tunaenda kukinukisha’ akisema kuwa Lissu alifafanua kauli hizo.

Katuga alipohoji kama Mnyika ameleta mahakamani hotuba hiyo inayofafanua maneno hayo, Mnyika alijibu: “Nimeileta kwa maelezo ya mdomo kwasababu si wajibu wangu kuthibitisha mashtaka”.

Katuga alijaribu kumjenga Mnyika kama shahidi mwenye masilahi binafsi (interested witness) katika kesi hiyo, kwa kuwa uteuzi wake kama Katibu Mkuu ulipendekezwa na mshitakiwa (Tundu Lissu), na kwamba yeye ndiye aliyeratibu kikao cha Kamati Kuu cha tarehe 29 Agosti 2026 kilichoazimia kumtetea Lissu kwa nguvu zote.

Mnyika alikataa vikali madai hayo akieleza kuwa masilahi yake katika kesi hiyo yanawakilisha masilahi ya chama (party interest) na masilahi ya umma (public interest), na siyo masilahi yake binafsi.

Kuhusu ushiriki wa vyombo vya habari katika mkutano wa watiania wa CHADEMA wa Aprili 3, 2025, Mnyika ameeleza kuwa CHADEMA iliwaalika waandishi wa habari kwa ujumla, akisisitiza kuwa chama kinaheshimu uhuru wa habari na hakikuwapa waandishi masharti wala angalizo lolote la kurusha au kutorusha matangazo ya moja kwa moja au ya kurekodiwa ya mkutano huo. Mnyika ameongeza kuwa jukumu la kusambaza taarifa hiyo lilikuwa chini ya uhuru wa vyombo vyenyewe vya habari na siyo kwa kulazimishwa na chama.

Kutokana na muda wa mahakama kumalizika, jopo la majaji liliahirisha kesi hiyo saa 11:00 jioni. Shauri hilo linatarajiwa kuendelea kesho yake, Jumanne, Septemba 1, 2026, ambapo Katibu Mkuu John Mnyika ataendelea kukabiliana na maswali ya dodoso.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!