Latest Posts

USHAHIDI WA MNYIKA JUU YA ‘NO REFORMS NO ELECTION’ AKIMTETEA LISSU

Kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Antiphas Lissu, inaendelea leo Jumatatu, Agosti 31, 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa chama hicho, John John Mnyika, amemaliza kutoa ushahidi wake wa utetezi kama Shahidi wa Pili wa Utetezi akimtetea Mwenyekiti wake dhidi ya mashtaka hayo mazito ya uhaini.

Mara baada ya kumaliza ushahidi wake wa msingi (examination-in-chief) asubuhi ya leo, jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dastan Ndunguru liliaamua kuahirisha shauri hilo hadi saa nane na nusu mchana ambapo Mnyika anatarajiwa kukabiliwa na maswali ya dodoso (cross-examination) kutoka kwa mawakili wa serikali.

Katika ushahidi wake, Mnyika ameendelea kudai kuwa tuhuma zote dhidi ya Lissu ni za “uongo na za kubambikiza” zenye lengo la kisiasa la kukwamisha mabadiliko ya kidemokrasia nchini.

Mnyika ameiambia mahakama kuwa shtaka linalomkabili Lissu linalodai kuwa yeye ndiye aliyetayarisha na kuitisha mkutano wa watia nia wa tarehe 3 Aprili 2025, pamoja na kuchapisha video yenye maneno yanayodaiwa kuwa ya uhaini kwenye Jambo TV, ni la uongo na lisilo na msingi wowote wa kisheria.

Mnyika amefafanua kuwa kama Mtendaji Mkuu na msimamizi mkuu wa uendeshaji wa CHADEMA, alishangazwa sana kusikia tuhuma hizo. Amesisitiza kuwa mkutano huo wa watia nia ulikuwa wa ndani na uliandaliwa kikamilifu chini ya maelekezo yake na kuongozwa na Sekretarieti ya chama ambayo yeye ndiye Mwenyekiti wake. Mwenyekiti wa chama (Lissu) si mjumbe wa Sekretarieti na hashiriki katika maandalizi ya namna hiyo, na wakati maandalizi hayo yote yakifanyika Mikocheni, Lissu alikuwa mbali kwenye ziara ya kikazi Kanda ya Nyasa.

Akijibu swali la Lissu kuhusu uhalali wa maneno kama “msimamo huu unaashiria uasi… tutakinukisha” na kuzuia uchaguzi, Mnyika ameweka wazi kuwa maneno hayo hayajengi kosa lolote la jinai.

Amerejea historia kwa kunukuu kauli maarufu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyewahi kuwataka vijana “kuasi” dhidi ya mifumo kandamizi, akibainisha kuwa Nyerere hakuwahi kukamatwa kwa kauli hiyo. Amesema kuwa hamasa ya “uasi” ni kukataa uovu, na “kuzuia uchaguzi” maana yake ni kutumia njia za kidemokrasia (kama kususia au kushinikiza kuahirishwa) ili kudai uchaguzi huru na wa haki, kwani kuzuia uchaguzi usio huru ni haki.

Mnyika amesema maneno yanayolalamikiwa hayajawahi kutaja neno “serikali” wala kuelekezwa kwa kiongozi yeyote maalum wa serikali, hivyo dhana ya kuwa yalilenga “kuitishia serikali” haina mashiko kisheria.

Katika kuelezea asili ya msimamo wa CHADEMA wa “No Reforms No Election”, Mnyika ameeleza kwa kirefu jinsi maridhiano kati ya CHADEMA na CCM yalivyokufa. Amesema mazungumzo hayo yaliyofanywa na timu zilizomjumuisha Mbowe na Kinana yaligonga mwamba baada ya CCM kukataa mapendekezo yote ya mabadiliko ya kikatiba kwa maandishi. Baada ya hapo, serikali ilipeleka bungeni miswada ya sheria ya uchaguzi mnamo Januari 2024, na Mnyika alipoenda kutoa maoni ya chama kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba na utawala alizuiliwa kabisa kuzungumzia masuala yanayohusu Katiba.

Amesema matokeo ya kukataa mabadiliko hayo yalijionesha kwenye kile alichokiita kuwa uozo wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Novemba 2024 uliosimamiwa na TAMISEMI chini ya Waziri Mohamed Mchengerwa. Mnyika amesema kuwa chaguzi hizo ziligubikwa na vurugu kubwa na hujuma, ikiwemo wagombea karibu wote wa upinzani kuenguliwa kwa sababu kama “hawajui kusoma na kuandika” au “si wakazi wa vijiji husika”, mawakala wa upinzani kuondolewa vituoni kwa nguvu ya polisi na mgambo.

Amesema uozo huo uliilazimu Kamati Kuu ya CHADEMA kukutana kwa dharura tarehe 2 na 3 Desemba 2024 na kupitisha maazimio 10, likiwemo la kutoshiriki uchaguzi mkuu wa 2025 bila mabadiliko ya kikatiba na kisheria. Azimio hilo la “No Reforms No Election” lilitangazwa na aliyekuwa Mwenyekiti Freeman Mbowe Desemba 10, 2024. Baadaye, Baraza Kuu la tarehe 20 Januari 2025 na Mkutano Mkuu wa tarehe 21 Januari 2025 yaliyokuwa chini ya uenyekiti wa Mbowe yalilipitisha azimio hilo kama sera rasmi ya chama. Tundu Lissu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya tarehe 22 Januari 2025 na kupewa jukumu la kuanza utekelezaji wake mara moja.

Aidha ameeleza kuwa Sekretarieti ya chama ilikaa Bagamoyo kati ya tarehe 31 Januari na 4 Februari 2025 kupanga mkakati wa kutoa elimu kwa umma kwa njia za amani na kidemokrasia, na walikutana na wadau mbalimbali ikiwemo asasi za kiraia kama TLS, Jaji Warioba, na viongozi wa dini.  Amesema hata Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Naibu wake Sisty Nyahoza, walithibitisha kuwa kaulimbiu ya “No Reforms No Election” ni ya kisiasa na haikiuki sheria yoyote.

Mnyika amedai kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kukamatwa kwa Lissu tarehe 9 Aprili 2025 mkoani Ruvuma na kampeni kubwa ya kisheria na kiserikali ya kujaribu kukiua chama cha CHADEMA. Amebainisha kuwa siku hiyohiyo Lissu aliyokamatwa, kesi ya madai ilifunguliwa mahakamani dhidi ya Katibu Mkuu na Bodi ya Wadhamini ya chama kuomba zuio la matumizi ya mali na shughuli za chama.

Amesema baadaye, mfululizo wa uonevu ulifuata ikiwamo Msajili kutengua uteuzi wa Katibu Mkuu, Manaibu, Sekretarieti, na wajumbe wa Kamati Kuu, Msajili kuzuia kutoa ruzuku kwa CHADEMA kwa madai kuwa hakuna Katibu Mkuu halali na Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi kutangaza kuifungia CHADEMA kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 na chaguzi zote hadi mwaka 2030, kwa kisingizio cha Katibu Mkuu kutosaini fomu ya maadili ya uchaguzi.

Mnyika ametoa wasifu wa Lissu akieleza kuwa amemfahamu kwa miaka 23 na kumtaja kama mtetezi shupavu wa haki na msimamo wa kweli, akisema kesi hii ni “mwendelezo wa serikali na vyombo vyake kubambikiza kesi dhidi ya viongozi wa CHADEMA kwa kutumia mahakama kama silaha ya kupambana na wapinzani na kukwamisha mabadiliko”. Alitolea mfano kesi ya ugaidi ya Mbowe ya mwaka 2021 iliyofutwa na DPP mwaka 2022 kama kielelezo cha mbinu hizi chafu za kisheria.

Shauri hilo linatarajiwa kuendelea mchana huu saa nane na nusu kwa ajili ya Mnyika kuanza kukabiliwa na maswali ya dodoso ya Jamhuri.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!