Timu ya mpira wa volleyball wanaume ya Manispaa ya Iringa imeibuka washindi wa kwanza katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Watumishi wa Serikali za Mitaa (SHIMISEMITA) kitaifa, yaliyofanyika jijini Mbeya mwaka 2026.
Mashindano hayo yalihusisha jumla ya Halmashauri 177 kutoka maeneo mbalimbali nchini, huku timu ya Manispaa ya Iringa ikionyesha kiwango kizuri na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa mchezo huo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Bi. Zaina Mlawa, alionyesha furaha kubwa pamoja na wanamichezo wa Manispaa hiyo baada ya timu yao kuibuka washindi wa kwanza katika mashindano hayo.

Ushindi huo unakuwa muhimu kwa Manispaa ya Iringa kutokana na historia ya mashindano hayo, kwani mwaka 2025 timu hiyo ilifika hatua ya fainali na kushika nafasi ya pili baada ya kukutana na timu iliyokuwa bingwa.
Kwa maana hiyo, matokeo ya mwaka huu yamekuwa “vice versa” na yale ya mwaka jana, ambapo timu ya Manispaa ya Iringa iliyokuwa mshindi wa pili mwaka 2025, sasa imefanikiwa kutwaa ubingwa mwaka 2026, huku timu iliyokuwa bingwa mwaka jana ikimaliza ikiwa mshindi wa pili.
Mafanikio hayo yanaonesha jitihada na maandalizi mazuri yaliyofanywa na timu ya Manispaa ya Iringa, pamoja na dhamira ya watumishi kushiriki kikamilifu katika michezo na kuendelea kuiwakilisha Manispaa hiyo katika mashindano ya kitaifa.
Ushindi huo pia umeongeza heshima kwa Manispaa ya Iringa katika medani ya michezo ya watumishi wa Serikali za Mitaa, huku timu hiyo ikitarajiwa kuendelea na maandalizi ili kulinda ubingwa huo katika mashindano yajayo.
