Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema utekelezaji wa Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovoti 220 kutoka Iganjo, Mkoani Mbeya, hadi Saza, Mkoani Songwe, pamoja na ujenzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Saza, utaimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa hiyo na kuchochea shughuli za uzalishaji, hususan uchimbaji wa madini katika Wilaya za Chunya na Songwe.
Akizungumza Septemba 11, 2026, katika Kijiji cha Saza, Wilaya ya Songwe, wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa utekelezaji wa mradi huo, Naibu Waziri wa Nishati amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza uzalishaji, kuendeleza kilimo cha kisasa na biashara, pamoja na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa umeme kwa wananchi na katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Aidha, amesema wakati Mradi wa Iganjo–Saza ukiendelea kutekelezwa, ni muhimu wananchi kufahamu maendeleo ya Mradi wa TAZA (Tanzania–Zambia Transmission Interconnector Project), ambao ni sehemu muhimu ya mipango ya Serikali ya kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa umeme na kukuza biashara ya umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.
“Napenda kuwahakikishia wananchi wa Songwe na Mbeya kwamba Serikali inaona changamoto za upatikanaji wa umeme katika maeneo yenu na inaendelea kuchukua hatua. Utekelezaji wa mradi huu ni kielelezo cha kuendelea kuhakikisha shughuli za kijamii na kiuchumi zinafanyika kwa ufanisi, huku tukijenga mfumo wa umeme ambao utaungana vizuri na kutoa uwezo mkubwa zaidi wa kusafirisha na kusambaza umeme,” amesisitiza Mhe. Salome.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, amepongeza kazi inayofanywa na Wizara ya Nishati kupitia TANESCO, akisisitiza kuwa mradi huo utakuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, ikiwemo kuibua fursa za ajira na kuchochea shughuli za uchimbaji wa madini.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Mhe. Balozi Zuhura Bundala, amesema TANESCO inaendelea kutekeleza jitihada za kujenga na kuboresha miundombinu ya umeme ili kwenda sambamba na kasi ya ongezeko la mahitaji ya nishati linalochochewa na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
“Utekelezaji wa mradi huu ni sehemu muhimu ya majukumu ya TANESCO ya kuendelea kujenga miundombinu ya umeme ili kumudu mahitaji ya sasa na ya baadaye. Tunahakikisha mradi huu unajengwa kwa ufanisi na kuendana na thamani ya fedha iliyowekwa,” alifafanua Mhe. Balozi Bundala.
Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, anayeshughulikia Mipango, Utafiti na Uwekezaji, Mha. Amos Joas, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, amesema utekelezaji wa mradi huo utagharimu Shilingi Bilioni 198.67 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18.
“Kwa sasa, maeneo ya Chunya na Songwe, hasa upande wa Mkwajuni, yanapata umeme kutoka Mkoa wa Mbeya kupitia Kituo cha Mwakibete kwa kutumia njia ya msongo wa Kilovoti 33 yenye urefu wa zaidi ya kilomita 116. Kutokana na umbali huo mrefu na ongezeko la mahitaji ya umeme, kumekuwa na changamoto katika upatikanaji wa umeme, hivyo utekelezaji wa mradi huu utasaidia kuboresha hali hiyo,” alieleza Mha. Joas.
Mkataba huo umesainiwa kati ya Serikali kupitia TANESCO na Mkandarasi Kampuni ya TBEA kwa ajili ya ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovoti 220 kutoka Iganjo, Mkoani Mbeya, hadi Saza, Mkoani Songwe, pamoja na ujenzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Saza.