Latest Posts

MWANACHADEMA ISHENGOMA, SAKATA LA TONETONE LILIVYOTIKISA MAHAKAMA MNYIKA AKIHOJIWA.

Kesi ya uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Antiphas Lissu, imeendelea mahakamani leo Jumanne, Septemba 1, 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.

Baada ya mapumziko ya mchana, mahakama ilirejea saa nane na dakika 54 mchana ambapo Katibu Mkuu wa CHADEMA, John John Mnyika, aliendelea kukabiliwa na maswali ya dodoso kutoka kwa mawakili wa upande wa mashtaka (Jamhuri).

Kwa siku ya leo mchana, upande wa mashtaka ulielekeza guvu zake katika kuchunguza masuala ya fedha na utendaji wa ndani wa CHADEMA. Mnyika alibainisha kuwa kama Katibu Mkuu, yeye ndiye msimamizi mkuu wa fedha (accounting officer) ambapo anaidhinisha maombi yote ya matumizi. Alieleza kuwa CHADEMA haiwalipi watendaji wake mishahara bali huwapa posho, na mara ya mwisho kulipa posho hizo ilikuwa ni mwezi uliopita. Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa malimbikizo ya madai ya posho kwa baadhi ya viongozi na watendaji wa sekretarieti kutokana na changamoto ya kuzuiliwa kwa rasilimali na ruzuku za chama kufuatia amri ya mahakama na msajili.

Kuhusu vyanzo vya fedha, Mnyika ameeleza kuwa kampeni yao ya uchangishaji fedha ya “Tonetone” ilikuwa imekusanya kiasi cha shilingi milioni 302 hadi mara ya mwisho alipoangalia kwa ajili ya Baraza Kuu na matumizi mahususi. Aliongeza kuwa michango mingine inatoka kwa Watanzania wa ndani na nje ya nchi (Diaspora) kupitia akaunti rasmi za benki ambazo zinapita kwenye mifumo rasmi inayoweza kufuatiliwa na mamlaka za nchi, akipinga wasiwasi wa upande wa serikali kuhusu uwezekano wa utakatishaji fedha.

Aidha, Wakili wa Serikali alimbana Mnyika kuhusu malalamiko ya mwanachama mmoja wa CHADEMA aitwaye Ishengoma Mtembe akidai kuwa Ishengoma aliita waandishi wa habari na kusema kuwa CHADEMA iliratibu mifumo maalumu ya mawasiliano ya kutumia pindi simu zinapozuiwa na kupanga njama za kusimamia vurugu na kuzuia uchaguzi mkuu wa Oktoba 29. Mnyika alijibu kwa msisitizo kuwa hamfahamu Ishengoma, hajawahi kusikia taarifa hizo, na chama chake hakikuhusika na mipango yoyote ya vurugu.

Kuhusu ripoti ya Tume ya Jaji Chande, Wakili wa Serikali alidai kuwa vurugu za uchaguzi zilipangwa na kuratibiwa, na kwamba baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa kwa uhaini kabla na baada ya uchaguzi huo walikiri polisi kuwa walifanya vurugu kufuatia kauli za Tundu Lissu. Mnyika alijibu kuwa anafahamu kuwa raia wengi walikamatwa na baadaye kuachiwa kwa maagizo ya Rais. Aliongeza kuwa CHADEMA haikubaliani kabisa na ripoti ya Tume ya Jaji Chande kuhusu matukio ya Oktoba 29, akisisitiza kuwa kusikia hotuba ya Jaji Chande haimaanishi kuikubali na ndiyo maana walihitaji tume huru ya uchunguzi ya kimataifa.

Wakili wa Serikali alihoji pia kuhusu uhalali wa mkutano wa Aprili 3, 2025 na kuhusu kama Lissu alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo au laa. Mnyika alifafanua kuwa mkutano huo ulilenga kuelimisha watia nia kuhusu msimamo wa No Reforms No Election. Mnyika alieleza kuwa yeye ndiye aliyefungua mkutano huo na kisha kumkaribisha Tundu Lissu kutoa mada. Aliongeza kuwa Lissu alizungumza kama Mwenyekiti wa chama na siyo Mwenyekiti wa mkutano, na kwamba Lissu ndiye alikuwa msemaji mkuu katika mkutano huo.

Hata hivyo, mfululizo wa maswali hayo ya dodoso ulikatishwa saa 11 kamili jioni kufuatia muda wa mahakama kuisha. Jopo la majaji liliamua kuahirisha shauri hilo hadi kesho yake asubuhi, Jumatano, Septemba 2, 2026, saa tatu kamili asubuhi ili kuendelea na maswali ya dodoso kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!