Latest Posts

KANISA LA ANGLIKANA LAONYA KUHUSU HALI MBAYA YA UCHUMI CHINI YA RAIS RUTO

Kanisa la Anglikana nchini Kenya limemwaga cheche kali likieleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali mbaya ya uchumi na huduma za umma nchini humo, likisisitiza kuwa hali inazidi kuwa ngumu chini ya uongozi wa Rais William Ruto huku wananchi wakiendelea kuteseka.

Akizungumza katika kikao cha mwaka huu cha Anglican Church Standing Committee of the Provincial Synod, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Kenya (ACK), Jackson Ole Sapit, amesema kuwa ni wakati wa Wakenya kusimama kidete na kudai uwajibikaji kutoka kwa Serikali kabla mambo hayajaharibika zaidi.

“Ukimya mbele ya mateso si kutokuwa na upande; ni kushiriki katika tatizo, lakini kupanda miti huku uking’oa haki ni unafiki,” alionya Askofu Ole Sapit.

Ameongeza kuwa mamilioni ya Wakenya wanakabiliwa na lindi la umaskini linalosababishwa na ukosefu mkubwa wa ajira, kupanda kwa gharama za maisha, kufungwa kwa biashara, na mzigo mzito wa kodi ambao hauna uwiano na rasilimali zinazorejeshwa kwa wananchi.

“Ni wakati wa kukubali kwamba nchi yetu inazidi kuwa mbaya. Mamilioni ya Wakenya wanaendelea kuteseka kutokana na ukosefu wa ajira, kupanda kwa gharama za maisha, biashara kufungwa na kuongezeka kwa mzigo wa kodi… Wakenya wanajiuliza kwa nini wanalipa kodi zinazowafanya wananchi kuwa maskini,” alidokeza.

Mbali na uchumi, Kanisa hilo limetupa lawama nzito katika sekta ya afya, likisema inakabiliwa na huduma duni, uzembe, na ukosefu wa uwazi, huku likitolea mfumo mpya wa bima ya afya kuwa haufanyi kazi ipasavyo.

“Changamoto zinazoendelea katika sekta ya afya zimefichua udhaifu wa mfumo na kusababisha mateso makubwa kwa wananchi. SHA haifanyi kazi; sekta ya afya iko katika hali mbaya,” alisisitiza Ole Sapit.

Aidha, katika sekta ya elimu, ACK imepinga vikali muswada uliopo bungeni unaolenga kuipa Serikali mamlaka ya kuchukua usimamizi wa shule zinazoendeshwa na taasisi za kidini, ikawataka wabunge kuachana nao mara moja.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!