Jumla ya watoto 493,680 Mkoani Kilimanjaro wamelengwa kupatiwa chanjo ya matone ya kuwakinga na ugonjwa wa polio ili kuhakikisha jamii inakuwa na kinga kamili dhidi ya ugonjwa wa polio.
Akizungumza Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro katika mafunzo ya uwezeshaji Wanahabari kuhusu umuhimu wa chanjo ya polio kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 10,Anne Shuma Afisa Mhamasishaji wa Chanjo ya Polio toka Wizara ya Afya amesema kuwa kampeni hiyo itatekelezwa katika mikoa yote nchini kwasababu ya mwingiliano mkubwa wa watu iliopo katika jamii kutokana na shughuli mbalimbali za kijamii,usafirishaji na kiuchumi ikiongozwa na kauli mbiu “Mpe chanjo,zuia polio”.
“Jamii inapaswa kufahamu kuwa polio ni ugonjwa hatari unaoweza kusababisha kupooza kwa ghafla kuliko tepetetepe,ulemavu wa kudumu na hata kifo kwani ugonjwa huu unasabishwa na virusi vya polio aina ya kwanza,ya pili na tatu” alisema
Shuma amesema kuwa ugonjwa huo huenea kwa njia ya kula chakula au kunywa maji yenye vimelea yaani virusi vya polio endapo kanuni za usafi hazizingatiwi katika jamii.
Amesema kuwa kampeni hiyo kwa Mkoa wa Kilimanjaro inatarajiwa kuanza Agosti 27 hadi 30 mwaka huu na kurudiwa Septemba 29 hadi Oktomba 2 mwaka huu kwa kuhusisha mikoa 8 ikiwemo Dar es salaam,Pwani,Tanga, Kilimanjaro,Arusha,Manyara, Dodoma na Mara.
Shuma amesisitiza kuwa kampeni ya chanjo hiyo itatekelezwa kwa wahudumu wa afya kupita nyumba kwa nyumba,vituo vya kutolea huduma ya afya na maeneo ya mikusanyiko ikiwemo shuleni,sokoni,nyumba za ibada,stendi za mabasi na maeneo mengine ngazi ya jamii.
Kwa upande wao Wanahabari waliopatiwa mafunzo hayo wameishukuru Wizara ya afya kwa kuwapatia elimu hiyo ili waweze kuifikisha kwa usahihi kwa jamii na kuondoa dhana potofu juu ya chanjo kwa kuongeza ushiriki wa wazazi na walezi kuwapatia watoto wao chanjo.
