Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku Tanzania imetangaza kuongeza bei elekezi ya zao la tumbaku kwa msimu wa kilimo wa 2026/2027 kutoka dola za Marekani 1.95 kwa kilo katika msimu uliopita hadi dola 2.05 kwa kilo, hatua inayolenga kuwapa motisha wakulima kuongeza uzalishaji na kuinua tija ya zao hilo.
Akizungumza siku ya Jumatano wakati akiwasilisha taarifa katika kikao cha Kamati ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, Stanley Mnozya, amesema ongezeko hilo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuendelea kuboresha sekta ya tumbaku na kuimarisha kipato cha wakulima.
Mnozya amewataka wakulima kuendelea kuzalisha tumbaku kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ili kuongeza ubora wa zao hilo na kunufaika zaidi na soko la ndani na la kimataifa.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Mkoa wa Tabora, Kaimu Mkuu wa Mkoa huo, Balozi Simon Sirro, amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 465 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika kipindi cha miezi sita iliyopita, huku akieleza kuwa sekta ya kilimo imeendelea kuimarika na kuchangia ongezeko la uzalishaji wa mazao mkoani humo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Said Nkumba, amesema chama hicho kitaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani ya CCM hususan katika sekta ya kilimo, ili kuhakikisha wakulima wanapata mazingira bora ya uzalishaji na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.