Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Dkt. Charles Kitima, ametoa wito kwa serikali na viongozi wa umma kuimarisha utamaduni wa kuwasikiliza wananchi, akisisitiza kuwa Watanzania ni watu wavumilivu ambao hawajazoea kutumia silaha wala kufanya vurugu katika kudai haki zao.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 13, 2026, kufuatia mkutano kati ya Maaskofu wa TEC na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan uliofanyika Agosti 10 Ikulu ya Chamwino, Padre Kitima amebainisha kuwa msingi wa utawala bora ni kutambua kuwa mamlaka yote yanatoka kwa wananchi.
Padre Kitima amekumbusha masharti ya Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoeleza kuwa utawala wa nchi uko chini ya wananchi na viongozi wamepewa dhamana tu ya kusimamia.
“Ukiwa kiongozi… lazima ukubali kuwasikiliza wananchi. Eh wananchi wanachosema kizuri kitamu lazima usikilize. Na huo ndio uwajibikaji… Sasa unapopora yale mamlaka kuwafanyia chochote unachotaka kwa kweli inakuwa ni kukosea utu wa Mtanzania na kukosea ubinadamu,” amesisitiza Padre Kitima na kuongeza,
“Watanzania ni watu waelewa ni watu wavumilivu hawajazoea kufanya vurugu kwa kutumia silaha… hata wale waandamanaji hata muwasemeje sikuona mwandamanaji aliyekamatwa na polisi akiwa na silaha. Labda hawakutuambia lakini walau wangekuwa na silaha tungeambiwa,” amesema kiongozi huyo wa kiroho.
Padre Kitima ameshauri serikali kufuata mifano ya nchi kama Afrika Kusini, ambazo zilivuka mkwamo wa kisiasa kwa njia ya mapatano, kukiri ukweli, na kusameheana bila lazima ya kupelekana mahakamani. Ameonya kuwa Tanzania isiwe “kisiwa” kinachojitenga na vigezo vya kimataifa vya haki za binadamu, kwani kufanya hivyo ni kujidhalilisha mbele ya jamii ya kimataifa.