Wananchi wa Kijiji cha Msasa, Kata ya Runzewe, Wilaya ya Bukombe, wameushukuru Mgodi wa Wachimbaji Wadogo wa Msasa kwa kuchangia maendeleo ya jamii kwa kujenga Kituo cha Polisi pamoja na Zahanati katika eneo hilo.
Wananchi hao wameeleza kuwa ujenzi wa Kituo cha Polisi utasaidia kuimarisha usalama katika eneo hilo, hususan kutokana na shughuli za uchimbaji madini zinazoendelea, huku Zahanati hiyo ikitarajiwa kupunguza adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati mapema leo wakiwa kwenye eneo hilo la ujenzi wa miradi hiyo, wananchi hao wamesema uwepo wa huduma hizo karibu na makazi yao utawasaidia kupata huduma muhimu kwa urahisi zaidi.
Msimamizi wa ujenzi wa majengo hayo mawili, Lifa Kikome, amesema miradi hiyo ipo katika hatua za mwisho za ujenzi, ambapo kwa sasa wanaendelea na kazi za kukamilisha milango pamoja na baadhi ya shughuli nyingine za mwisho.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Msasa, George Otieno, amesema uamuzi wa kujenga Zahanati na Kituo cha Polisi umetokana na mahitaji yaliyowasilishwa na wananchi, ambao walieleza kuwa huduma hizo ni miongoni mwa vipaumbele vyao.
Amesema wananchi walikuwa wameanza ujenzi wa Zahanati hiyo, hivyo mgodi huo ukaona umuhimu wa kuunga mkono jitihada hizo na kuhakikisha mradi huo unakamilika, sambamba na kujenga Kituo cha Polisi kwa ajili ya kuimarisha usalama katika eneo hilo.
