Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, ameongoza shughuli ya Evening Jogging ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha wananchi kushiriki na kuunga mkono Mashindano ya Michezo ya Wanafunzi wa Shule za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSA) 2026 yatakayofanyika mkoani humo.
Malima amesema lengo la mashindano hayo ni kuibua na kuinua vipaji vya wanafunzi katika michezo, pamoja na kuimarisha ushirikiano na mshikamano miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ameeleza kuwa zaidi ya wanamichezo 6,000 kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi wanatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo, jambo litakaloiwezesha Morogoro kunufaika kiuchumi kupitia ongezeko la wageni watakaofika mkoani humo.
