Latest Posts

WAZIRI MAVUNDE AAGIZA MASOKO YA MADINI KUWA WAZI MPAKA USIKU KURAHISISHA HUDUMA KWA WATEJA

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameiagiza Tume ya Madini kuongeza muda wa uendeshaji wa masoko ya madini mpaka saa 3:00 usiku, hatua inayolenga kuongeza fursa za biashara na kuwahudumia wafanyabiashara na wauzaji wa madini kwa muda mrefu zaidi ili kuendana na mahitaji ya wadau na kuongeza ufanisi katika biashara ya madini.

Mavunde ametoa agizo hilo Agosti 11, 2026, wakati akijibu maswali ya Wabunge katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma, ambapo Wizara imewasilisha taarifa kuhusu hali halisi na maendeleo ya sekta ya madini nchini.

Mavunde amesema Serikali pia inaendelea kuimarisha udhibiti wa biashara ya madini na utoroshaji, huku ikisisitiza uongezaji thamani ndani ya nchi. Ameeleza kuwa katika eneo la Mirerani, serikali itatekeleza mkakati ambao imejiwekea wa kukuza biashara hiyo ya madini ya Tanzanite kwa kuhakikisha mfumo wa biashara ya madini hayo unapitiwa ili kusaidia kuchochea ukuaji wa biashara ya madini ya Tanzanite.

Kuhusu uwekezaji, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua dhidi ya wenye leseni wanaoshikilia maeneo makubwa bila kuyaendeleza, akisisitiza kuwa maeneo yasiyoendelezwa kwa mujibu wa sheria yanaweza kuchukuliwa hatua, ikiwemo kufutwa kwa leseni. Aidha, Serikali inaendelea kushirikiana na Wizara ya Nishati kuhakikisha maeneo ya migodi yanapata umeme wa uhakika pamoja na kuzingatia miundombinu ya kimkakati katika mipango ya maendeleo.

Amesema Serikali pia inaendelea kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa madini kupitia mpango wa MBT unaolenga vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum. Kwa upande mwingine, Serikali imesaini hati za makubaliano 14 na wawekezaji ambao miradi yao bado haijaanza uzalishaji, huku ikiendelea kuweka mazingira wezeshi kwa taasisi za fedha kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo wenye sifa.

Akitoa taarifa ya hali ya sekta hiyo, Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, amesema madini yanaendelea kuwa sekta muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika mwaka wa fedha 2025/26, dhahabu iliongoza kwa uzalishaji baada ya kufikia tani 67.8 zenye thamani ya Sh trilioni 18.4. Aidha, kilogramu 28,701 za dhahabu ziliuzwa katika viwanda vitano vya kusafisha dhahabu nchini, ambapo kilogramu 21,710, sawa na asilimia 75.64, zilinunuliwa na Benki Kuu ya Tanzania.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, ameipongeza Wizara kwa hatua zinazochukuliwa kuimarisha sekta hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kudhibiti utoroshaji wa madini na kupunguza tozo katika mnyororo wa biashara ya madini na kuitaka Serikali iangalie upya tozo kwa wachimbaji wadogo ambazo zimekuwa ni mzigo mkubwa.

Naye Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, amesema Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) na kuhakikisha shughuli za madini zinawanufaisha wananchi wanaozunguka maeneo ya migodi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!