Airtel Money imezindua kampeni mpya ya miezi mitatu ijulikanayo kama “Minyoosho Inaendelea na My Airtel App”, inayolenga kuwazawadia wateja wanaotumia My Airtel App kufanya miamala ya kila siku huku ikihamasisha matumizi ya huduma za kifedha kidijitali kwa urahisi na usalama.
Kupitia kampeni hiyo, kila mteja anayefanya muamala kupitia My Airtel App hupata nafasi ya kuzungusha gurudumu la kidijitali (Spin & Win) na kujishindia zawadi mbalimbali papo hapo, zikiwemo pikipiki, runinga, simu janja, fedha taslimu na zawadi nyingine.
Ili kushiriki, mteja anatakiwa kutumia My Airtel App kufanya miamala mbalimbali ikiwemo kutuma fedha, kufanya malipo, kununua muda wa maongezi, vifurushi vya intaneti, kulipa bili, kufanya miamala ya kimataifa pamoja na kulipia huduma ya Home Broadband.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Airtel Money Tanzania, Andrew Rugamba, alisema kampeni hiyo inalenga kuongeza matumizi ya My Airtel App na kuwapa wateja motisha wa kutumia huduma za kifedha kidijitali.
“Kupitia kampeni yetu ya Minyoosho Inaendelea na My Airtel App, tunataka kuona wateja wetu wanahamasika kutumia App kufanya miamala yao ya kila siku. Kila muamala utampa mteja nafasi ya kushinda zawadi papo hapo,” alisema Rugamba.
Aliongeza kuwa Airtel ni miongoni mwa kampuni zilizoanzisha matumizi ya mfumo wa michezo ya zawadi (gamification) katika huduma za kifedha kidijitali, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika uchumi jumuishi wa kidijitali.
Aidha, Airtel Money imewataka wateja kuwa waangalifu dhidi ya utapeli, ikisisitiza kuwa washindi wote watawasiliana kupitia namba rasmi ya huduma kwa wateja ya 100 pekee na kupokea ujumbe rasmi wa SMS.
Pia imewataka wateja kutotoa namba zao za siri (PIN), namba za uthibitisho (OTP) au taarifa nyingine binafsi kwa mtu yeyote anayejitambulisha kuwa mfanyakazi wa Airtel kupitia namba zisizo rasmi.
Kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa “Airtel Kila Kona”, unaolenga kusogeza huduma za kidijitali kwa Watanzania wote mijini na vijijini kupitia teknolojia rahisi na salama.