Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuwawezesha Watanzania kujiletea maendeleo, ikiwemo kurekebisha sheria mbalimbali zinazowakwaza katika kutekeleza shughuli zao.
Ameyasema hayo leo, Ijumaa, Oktoba 2, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mwibara, eneo la Kibara, mkoani Mara. Amesema baadhi ya mambo yamefanyika ndani ya siku 100 kama alivyoahidi Rais, huku mengine yakiendelea kuchukuliwa hatua.

“Leo tunavyoongea, tumerekebisha sheria mbalimbali ili tuweze kuhakikisha kuwa Watanzania hawakwazwi na baadhi ya sheria katika kutekeleza wajibu wao,” amesema.
Amesema miongoni mwa hatua hizo ni kuwapa wafanyabiashara wapya muda wa kuimarisha biashara zao, ambapo kodi ya mapato kwa biashara mpya inaanza baada ya mwaka mmoja tangu kupata TIN kwa ajili ya kuanza biashara.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekemea tabia ya baadhi ya watumishi kuwachangisha wananchi fedha kwa ajili ya mafuta ya magari ya wagonjwa (ambulance), akisema vitendo hivyo havikubaliki.

“Hatuwezi tukawa na magari ya Serikali yana mafuta, halafu ambulance ya kunusuru maisha ya wagonjwa tuchangishane mafuta. Haya ni mazoea mabaya ambayo hatutaki kuwa utaratibu wa Serikali. Wa aina hiyo akipatikana, tunachukua hatua kali,” amesema.
Aidha, amekemea tabia ya kuficha dawa zilizotolewa na Serikali huku wagonjwa wakielekezwa kununua dawa nje ya vituo vya afya, na kuwaagiza viongozi wa afya kufuatilia hali hiyo hatua kwa hatua ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazostahili.
Katika sekta ya nishati, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kusogeza huduma ya umeme kwenye vitongoji, mitaa na maeneo mapya ya makazi, akisisitiza kuwa wananchi katika maeneo hayo wanapaswa kunufaika na huduma hiyo.

Kuhusu mvua, amewataka viongozi na mamlaka zinazohusika kujiandaa kukabiliana na uwezekano wa mvua kubwa, ikiwemo kusafisha mifereji na maeneo ya kupitisha maji ili kupunguza athari za mafuriko.
Aidha, amewataka wananchi kutotumia nguvu au kuchukua sheria mkononi katika kushughulikia migogoro ya ardhi na mifugo, akisema Serikali inaendelea kuchukua hatua za kutatua changamoto za maeneo ya malisho na upatikanaji wa maji kwa mifugo.
Waziri Mkuu pia amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani ya nchi na mali za umma, akisisitiza kuwa shule, barabara na vituo vya afya ni mali za wananchi na uharibifu wake unawaathiri wao wenyewe.