Latest Posts

BAGONZA AWATAJA WANAOZUIA KATIBA MPYA

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dkt. Benson Bagonza, amesema wanaokwamisha kupatikana kwa Katiba Mpya ni makundi mawili ambayo ni wana CCM wanaomchukia mwana CCM mwenzao anayetoa matumaini ya katiba, pamoja na wapinzani wanaokimbilia katiba kabla ya kufanya maridhiano ya kweli.

​Dkt. Bagonza ameeleza hayo Agosti 4, 2026, kupitia ukurasa wake wa Facebook, akibainisha kuwa majibu hayo yanatokana na maswali aliyojiuliza kuhusu hotuba ya Katiba Mpya, na kusisitiza kuwa mchakato huo unahitaji maridhiano ya dhati badala ya mihemko ya kisiasa.

​”Maswali niliyouliza kuhusu hotuba ya katiba mpya yamejibiwa. Wanaozuia katiba mpya ni makundi mawili. kwanza, ni wana CCM wanaomchukia mwana CCM anayewapa watu matumaini ya katiba mpya. Pili, ni wapinzani wanaokimbilia katiba mpya kabla ya maridhiano ya kweli.” Ameandika Askofu Bagonza.

​Kiongozi huyo ametoa wito kwa wana CCM kuweka akiba ya maneno, kufuatia mijadala iliyoibuka kabla na baada ya vikao vya chama hicho vilivyofanyika Zanzibar tarehe 28 na 29 Julai, 2026, akionya kuwa baadhi ya kauli zimevuka mipaka ya heshima kwa viongozi wakuu.

​Askofu Bagonza ameeleza kuwa ni hatari kwa wanachama kujifanya wanahisi kuzorota kwa mahusiano kati ya Rais, Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu, na akawasihi kuacha tabia ya kuleta hoja za kutaka kujua mambo zaidi ya viongozi hao wanavyojuana.

​Amesisitiza kuwa mfumo wa Urais na Umakamu hautenganishwi, hivyo kumkashifu Makamu wa Rais ni sawa na kumkashifu Rais mwenyewe, huku akiwakumbusha wana CCM kutotumia kauli zitakazowakosesha ushawishi au pa kuweka uso baada ya migogoro hiyo kumalizika.

​Ameongeza kuwa Rais na Makamu wa Rais wakiishaapishwa wanakuwa mali ya Watanzania wote na si ya CCM pekee, akimweleza Makamu kama msaidizi na sauti ya Rais, na kusema ni Rais pekee mwenye haki isiyohojiwa ya kutilia mashaka jinsi anavyosaidiwa.

​Dkt. Bagonza amewasihi viongozi hao wawili kutambua kuwa wanaongoza nchi iliyojeruhiwa inayohitaji kutunzwa, akizitaka chokochoko za ndani ya chama kurudi nyuma na kujielimisha kutokana na hekima iliyotumika wakati wa kuingiza mfumo wa mgombea mwenza.

​Ametahadharisha kuhusu ajenda ya vijana wa rika la Gen Z akisema suala lao ni zito na halipaswi kuishia kwenye kuunda wizara au kutoa mikopo, bali linahitaji kusikilizwa kwa dhati badala ya kuwatumia.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!