Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dk. Jim Yonazi, amewaasa vijana kulinda afya zao na kuepuka tabia hatarishi ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU, akisisitiza kuwa vijana ni miongoni mwa makundi yaliyo hatarini zaidi nchini Tanzania.
Dkt. Yonazi ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa afua za UKIMWI katika Wilaya ya Uvinza, Mkoa wa Kigoma.

Aidha, Dk. Yonazi amesisitiza kuwa vijana ni nguvu kazi muhimu inayotegemewa na Taifa katika shughuli za uzalishaji mali na maendeleo, hivyo, amewataka kuendelea kujilinda na kuwalinda wengine kwa kutambua hali zao za kiafya na endapo watagundulika kuwa na maambukizi ya VVU, kuanza kutumia dawa mapema.
“Mnafanya kazi nzuri sana, endeleeni kuchangamkia uwepo wa mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa zenu ili kuwafikia wateja wengi zaidi na kujitangaza kitaifa na kimataifa,” amesisitiza Dk. Yonazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Adam Mrisho,alisisitiza kuwa Tume itaendelea kuwawezesha vijana kiuchumi na kuwajengea uwezo ili kuendeleza mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU nakupongeza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya hatua zinazolenga kufikia lengo la kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
