Wananchi wa Jimbo la Moshi Mjini wanatarajiwa kunufaika zaidi na huduma za kijamii baada ya kukabidhiwa magari yatakayosaidia usafiri katika shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kuwahudumia wagonjwa na familia zinazokabiliwa na misiba.
Utekelezaji huo umetokana na ahadi binafsi za Mbunge wa jimbo hilo, Ibrahim Shayo, alizozitoa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi magari hayo mjini Moshi, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, alimpongeza Shayo kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi zake kwa wananchi, akisema hatua hiyo ni mfano wa uongozi unaowajibika, unaojali wananchi na unaojenga imani kwa wapiga kura.
Mchengerwa alisema viongozi wengi hutoa ahadi nyingi wakati wa kampeni, lakini utekelezaji wake huwa wa kusuasua, hali inayowafanya wananchi kuwawajibisha kupitia uchaguzi. Alisisitiza kuwa viongozi wanaotekeleza ahadi zao hujenga uhusiano mzuri na wananchi na kuongeza imani kwa uongozi.

Kwa upande wake,Ibrahim Shayo alisema mbali na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliahidi kutumia fedha na uwezo wake kutekeleza ahadi binafsi, ikiwemo kutoa mabasi mawili aina ya Costa kwa shughuli za kijamii, pamoja na kununua gari la kubeba wagonjwa (ambulance) na gari la kubebea miili, ahadi ambazo amesema sasa zote zimekamilika.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alisema utekelezaji wa ahadi hizo unaonesha dhamira ya kweli ya kuwahudumia wananchi na unapaswa kuwa mfano kwa viongozi wengine, akibainisha kuwa wananchi wanathamini zaidi matendo kuliko maneno.
