Latest Posts

LISSU AIBUA MADAI YA ‘KUNYIMWA’ NAKALA YA HOTUBA YA JAJI CHANDE KUHUSU MATUKIO YA OKT. 29

Shauri la Kikatiba Na.7300/2026 lililofunguliwa na Mawakili Kulwa William Maduhu, Nashon Nkung na Paul Kisabo dhidi ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) na wenzake linaendelea kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu Dodoma mbele ya jopo la Majaji watatu (3) wakiongozwa na Jaji Amir Mruma.

Katika shauri hilo, ambalo vikao vyake vya usikilizwaji vinafanyika kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam waleta maombi waliojitambulisha kwenye kesi hiyo kuwa ni Mawakili wa Tundu Lissu wanalalamikia kuzuiliwa na/au kukosa haki ya faragha wanapokwenda kumuona mteja wao gerezani Ukonga.

Wakati akihoji maswali ya dodoso (cross examination) kwa shahidi wa pili (2) wa waleta maombi Nashon Nkung, Tundu Lissu ambaye ni mjibu maombi wa nne (4) shauri hilo licha ya kueleza kuunga mkono hoja zote zilizoletwa Mahakamani hapo na waleta maombi, amegusia namna maafisa wa magereza walivyokataa kumpatia nakala ya hotuba ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea Nchini Oktoba 29.2025 (Siku ya Uchaguzi Mkuu) na siku zilizofuata Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman aliyowasilisha wakati anakabidhi ripoti ya tume hiyo

Lissu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa amesema aliwaagiza Mawakili wake wamletee nakala hiyo, kutokana na kwamba katika kesi ya uhaini inayomkabili upande wa Jamhuri umefungua maombi madogo ya kumuongeza shahidi ambaye kwa namna moja au nyingine endapo maombi hayo yatakubaliwa yeye (Lissu) atajumuishwa moja kwa moja na matukio ya vurugu za Oktoba 29.2025 na siku zilizofuata.

Anasema licha ya kwamba vurugu hizo zilitokea ikiwa miezi sita (6) tangu awe gerezani, lakini analazimika kujiandaa na utetezi, na kwamba aliwaagiza Mawakili wake kumpelekea nyaraka hiyo kama sehemu ya maandalizi ya utetezi wake, lakini licha ya Mawakili kufanya hivyo maafisa wa Magereza wameizuia na hawajamkabidhi hadi leo,

Kwa upande wake, Nkung ambaye alikuwa shahidi wa kwanza leo, Jumanne tarehe 21/07/2026 ameieleza Mahakama namna maafisa wa Magereza Ukonga wanavyompekua, kumpa onyo na kumnyima faragha ya kuzungumza na mteja wake, jambo ambalo amesema ni kinyume cha miongozo, sheria, na kanuni zinazosimamia mawakili na magereza.

Katika hatua nyingine, Lissu amegusia namna viongozi waandamizi wa CHADEMA kama vile John Heche, John Mnyika, Amani Golugwa na baadhi ya Mawakili wake akiwemo Dickson Matata, Deogratias Mahinyila na Gaston Garubindi walivyopigwa marufuku kwenda kumuona gerezani, jambo ambalo linamnyima nafasi ya kuandaa utetezi wake kwakuwa baadhi yao ni sehemu ya mashahidi wake kwenye kesi ya uhaini inayomkabili.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!