Mwaka 2026 unatajwa kuwa mwaka wa mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini Tanzania, huku viongozi kutoka sekta ya umma na binafsi wakitarajiwa kuwa injini ya mabadiliko hayo kupitia uamuzi, sera na uwekezaji mkubwa wenye athari chanya kwa uchumi wa taifa. Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na gazeti la The Citizen Januari 2, 2026, viongozi kadhaa wametambuliwa kuwa na nafasi muhimu katika kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) na kuvutia mitaji ya kigeni.
Katika sekta binafsi, Edha Nahdi, Mkurugenzi Mtendaji wa Amsons Group, ametajwa kuwa miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa zaidi wa kiuchumi kwa mwaka 2026, kutokana na kasi ya upanuzi wa uwekezaji wake ndani na nje ya Tanzania. Hatua hizi zinaelezwa kuendana na mwelekeo wa taifa wa kupanua wigo wa viwanda na kuimarisha uchumi unaojitegemea.
Nahdi, anayeongoza himaya ya Amsons Group, ametajwa kama mfano wa mafanikio ya biashara za kizalendo zilizopevuka na kuvuka mipaka ya kitaifa. Chini ya uongozi wake, Amsons imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta za nishati, uzalishaji wa saruji kupitia viwanda ikiwamo Mbeya Cement, pamoja na usafirishaji, hatua zilizoongeza ajira na mapato ya serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali.
Mwaka 2024, Nahdi aliweka historia baada ya Amsons Group kuinunua Kampuni ya Bamburi Cement ya Kenya kwa takriban Dola za Marekani milioni 180, sawa na shilingi bilioni 475 za Kitanzania. Ununuzi huo umetajwa kuwa uwekezaji mkubwa zaidi kuwahi kufanywa na Mtanzania nje ya nchi, hatua iliyotajwa kuimarisha hadhi ya wawekezaji wa Kitanzania kimataifa.
Mapema Desemba 2025, Amsons Group ilitangaza kuingia katika ushirikiano wa kimkakati na kampuni ya Exergy Africa Limited ya Zambia kwa ajili ya kujenga na kupanua miradi ya uzalishaji na miundombinu ya nishati nchini humo. Mradi huo unatarajiwa kuzalisha megawati 1,000 za umeme wa jua na megawati 300 za umeme wa makaa ya mawe, kwa uwekezaji wa jumla wa Dola milioni 900, ambapo Dola milioni 600 zitaelekezwa kwenye nishati ya jua na Dola milioni 300 kwenye umeme wa makaa ya mawe.

Kwa mujibu wa Nahdi, biashara si suala la faida pekee bali ni chombo cha kuifanya Tanzania kuwa kiongozi wa kikanda kiuchumi na kiviwanda. Alikariri akisema, “Tanzania ina vipaji, rasilimali, na eneo la kimkakati la kuongoza mapinduzi ya viwanda kikanda. Lengo letu ni kubadilisha viwanda vya ndani na kuhakikisha biashara za Kitanzania zinakuwa viongozi na si wafuasi.”
Nahdi pia amesisitiza umuhimu wa ukuaji wa uchumi unaozingatia mazingira na ustawi wa jamii, akibainisha kuwa kila mradi wa viwanda unapaswa kuacha alama chanya kwa mazingira na wananchi wanaouzunguka. Ameeleza kuwa matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira na uwajibikaji wa kijamii ni nguzo kuu za uwekezaji endelevu.
Amsons Group, inayomilikiwa na kuendeshwa na familia ya Nahdi, kwa sasa inafanya biashara katika nchi kadhaa barani Afrika ikiwemo Tanzania, Zambia, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi, huku ikiajiri zaidi ya watu 10,000. Kampuni hiyo inatarajiwa kuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa saruji katika Afrika Mashariki, hali itakayoongeza ushindani na kupunguza gharama za ujenzi.
Nahdi anaona ujumuishaji wa kikanda kama fursa na wajibu wa pamoja, akisisitiza kuwa mipaka ya nchi haipaswi kuwa kikwazo cha maendeleo ya kiuchumi akibainisha kuwa, “Mipaka haipaswi kuwa vikwazo. Dhamira yetu ni kuunganisha masoko, kuunda ajira na kuimarisha nafasi ya Tanzania, huku tukihakikisha manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wetu.”
The Citizen imeeleza kuwa mwaka 2026 unatarajiwa kuwa wa mafanikio makubwa zaidi kwa Nahdi kutokana na mipango yake ya kupanua viwanda vya saruji na nishati, sekta ambazo ni mhimili wa maendeleo ya miundombinu ya taifa. Uwezo wake wa kusimamia miradi mikubwa unatambuliwa kama kichocheo kitakachowavutia wawekezaji wengine wa kimataifa kuona fursa zilizopo Tanzania.
Katika orodha hiyo ya viongozi wenye ushawishi wa kiuchumi kwa mwaka 2026, The Citizen pia imemtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kutoka sekta ya umma, ikibainisha kuwa jitihada zake katika diplomasia ya kiuchumi na kuimarisha mazingira ya biashara zimeendelea kufungua milango kwa wawekezaji wa kimataifa na kuimarisha mwelekeo wa uchumi wa nchi.