Wanafunzi wenye mahitaji maalum na wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini katika Kata ya Kalangalala Wilayani Geita wamepata tabasamu baada ya kupokea vifaa mbalimbali vya shule vilivyotolewa na Diwani wa kata hiyo Reuben Sagayika kwa lengo la kuwawezesha kuendelea na masomo yao bila vikwazo.
Vifaa hivyo vilivyotolea na madaftari pamoja na kalamu , vimetolewa na diwani wa kata hiyo kwa lengo ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusaidia wanafunzi na kupunguza changamoto za upatikanaji wa mahitaji ya msingi ya shule.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Sagayika amesema ugawaji wa vifaa hivyo unalenga kuimarisha mazingira bora ya kujifunzia na kuchochea ufaulu kwa wanafunzi, hususan wale wanaokabiliwa na changamoto za kiuchumi.

Kwa upande waka Kaimu Afisa elimu wa Kata hiyo Regina Kitau pamoja na mtendaji wa kata hiyo Emmanuel Bomani wamesema msaada huo utapunguza mzigo kwa familia nyingi na kuwahamasisha wanafunzi kuongeza bidii katika masomo yao.
Nao baadhi ya wazazi na walezi ambao watoto wao wamenufaika na vifaa hivyo wamemshukuru diwani kwa moyo wa kujitoa kusaidia vifaa hivyo.
Kwa ujumla, wadau wa elimu wameendelea kutoa wito kwa taasisi na watu binafsi kujitokeza kusaidia sekta ya elimu, wakieleza kuwa uwekezaji katika elimu ni msingi muhimu wa maendeleo ya Taifa.
