Na Theophilida Felician, Kagera.
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya majini, wasafiri na wavuvi katika Ziwa Victoria kuzingatia kanuni za usalama, huku likionya dhidi ya tabia ya kukagua vyombo vikiwa katikati ya maji safari ikiendelea.
Wito huo umetolewa na Mfawidhi wa TASAC mkoa wa Geita, Bw. Godfrey Mtwena Chegere, wakati akishiriki kikao cha umoja wa wamiliki wa boti kilichofanyika mwalo wa Magalini, wilayani Muleba. Chegere amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mmiliki kuhakikisha boti za abiria, mizigo na uvuvi zinakuwa na vifaa vya uokoaji, hususani majaketi ya kuokolea maisha (Life Jackets).

Katika hatua nyingine, Chegere amegusia mgogoro wa kisheria na kiusalama unaohusu ukaguzi wa vyombo vikiwa safarini. Amekumbusha kuwa sheria haziruhusu chombo kukaguliwa katikati ya maji kwani kitendo hicho kinaweza kusababisha ajali, hasa kwa boti ndogo, na kushauri kuwa busara itumike kwa kufanya ukaguzi katika maeneo maalum yaliyopangwa.
“Kusimamisha chombo katikati ya maji kwa ajili ya ukaguzi kunaweza kuleta madhara makubwa ikiwemo ajali. Tunapaswa kuzingatia sheria na kutumia busara katika utekelezaji wa majukumu yetu ya usalama,” alisema Chegere.
Hata hivyo, kikao hicho kiligubikwa na malalamiko kutoka kwa wamiliki wa boti wakiongozwa na Katibu wa umoja huo, Masudi Ibrahim Masudi, walioelezea kero ya kusimamishwa mara kwa mara na Maafisa Uvuvi wakiwa safarini. Walidai kuwa ukaguzi huo unaolenga kubaini biashara za magendo na samaki wachanga unahatarisha usalama wao, mbali na kulalamikia tozo ya shilingi 10,000 wanayotakiwa kulipa.
Akijibu malalamiko hayo, Afisa Mfawidhi wa Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi Muleba, Stanslaus Rwezaula, amesema kuwa wanalazimika kuwa makini zaidi na kufanya ukaguzi hata safarini baada ya kubaini baadhi ya wamiliki wa boti kushirikiana na wahalifu kusafirisha samaki wachanga.
Baada ya majadiliano, washiriki hao kutoka mikoa ya Geita na Kagera wamekubaliana kuwa, kama hakuna ulazima wa kipekee, ukaguzi ufanyike kabla ya chombo kung’oa nanga au baada ya kutia nanga mwalo ili kuepusha sintofahamu na ajali zisizo za lazima.
