Serikali za Denmark na Greenland zimeonesha msimamo usiotikisika dhidi ya matamanio ya Rais Donald Trump wa Marekani kutaka kukichukua kisiwa cha Greenland, zikisisitiza kuwa eneo hilo litaendelea kuwa sehemu ya Ufalme wa Denmark na mwanachama wa NATO na Umoja wa Ulaya.
Siku ya Jumanne, Januari 13, 2026, Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, na Waziri Mkuu wa Greenland, Jens-Frederik Nielsen, walikutana jijini Copenhagen kuonesha mshikamano wao usiku wa kuamkia mikutano mizito inayotarajiwa kufanyika leo Jumatano jijini Washington.
“Tunasimama pamoja na raia wa Greenland. Tunachagua Jamhuri ya Denmark, NATO, na Umoja wa Ulaya badala ya Marekani,” alisema Frederiksen wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, akijibu wito wa hivi karibuni wa Trump aliyedai kuwa ni lazima Marekani iidhibiti Greenland kwa njia yoyote ile.
Wakati viongozi hao wakitoa kauli hiyo, Mawaziri wao wa Mambo ya Nje, Lars Løkke Rasmussen (Denmark) na Vivian Motzfeldt (Greenland), wamewasili Ikulu ya White House leo kwa mazungumzo na Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, na Waziri wa Mambo ya Nje, Marco Rubio.
Mvutano huu unatokana na umuhimu wa kijiografia wa Greenland katika eneo la Aktiki (Arctic), ambapo Marekani inahofia ushawishi wa Urusi na China. Hata hivyo, Denmark imesisitiza kuwa ulinzi wa kisiwa hicho tayari upo chini ya mwavuli wa NATO na hakuna haja ya kile Trump alichokiita “makubaliano ya kukichukua” kisiwa hicho.