Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, inatarajiwa kuanza kusikilizwa mfululizo kuanzia tarehe 9 Februari hadi tarehe 6 Machi, 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa CHADEMA Taifa, Gaston Garubindi, amethibitisha kupitia mtandao wa X kuwa Lissu tayari amepokea taarifa rasmi kutoka kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu kuhusu ratiba hiyo mpya. Kesi hiyo, yenye namba 19605/2025, inasikilizwa na jopo la majaji watatu: Mhe. Dunstan Ndunguru, Mhe. James Karayemaha, na Mhe. Ferdinand Kiwonde.
Kesi hii, ambayo ilisitishwa tangu Novemba 12, 2025, kutokana na likizo ya mwisho wa mwaka ya mahakama, inatokana na tuhuma za uhaini zilizoelekezwa dhidi ya Lissu mwezi Aprili 2025. Tangu kuanza kwake, shauri hili limevuta hisia kali ndani na nje ya nchi, likichochea mijadala kuhusu uhuru wa kisiasa, nafasi ya vyama vya upinzani, na haki ya kisheria kwa viongozi waandamizi wa kisiasa nchini.
Lissu, ambaye anajisimamia mwenyewe mahakamani, amekuwa akisisitiza kuwa mchakato huo uwe wa wazi na uendelee bila ucheleweshaji usio na lazima, akiegemea haki za kikatiba na misingi ya utawala wa sheria. Shauri hili limeshapita katika hatua mbalimbali za awali, ikiwemo hoja za upande wa mashtaka na utetezi, pamoja na maamuzi ya mahakama kuhusu mapingamizi yaliyowasilishwa wakati wa vikao vilivyopita.