Latest Posts

KUELEKEA MSIMU WA 2026/2027: MTWARA YAWEKA MIKAKATI YA KUZUIA DHULUMA KWA WAKULIMA WA KOROSHO; MAADILI YASISITIZWA.

Mamlaka ya mkoa wa Mtwara zimeanza kuelekeza nguvu katika uwajibikaji wa vyama vya ushirika, kufuatia ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima wa korosho kwa msimu wa 2025/2026.
Maelekezo hayo yametolewa kwa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika mkoani humo, yakitaka hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya baadhi ya Vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) vilivyoshindwa kukamilisha malipo kwa wakulima.
Agizo hilo limetolewa wilayani Tandahimba na Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Michael Mtenjele, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, wakati wa Mkutano Mkuu wa 31 wa TANECU.
Katika maelekezo yake, Mtenjele amesisitiza umuhimu wa kukamilisha mchakato wa kuwachukulia hatua wahusika kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa kilimo wa 2026/2027, akibainisha kuwa kurejeshwa kwa fedha za wakulima ni jambo lisilopaswa kucheleweshwa.
Kwa upande mwingine, changamoto za uadilifu ndani ya baadhi ya AMCOS zimeendelea kujitokeza, hasa katika ngazi ya uongozi wa vyama vya msingi. Hali hiyo imeelezwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Newala, Alhaj Mwangi Kundya, ambaye amesisitiza umuhimu wa viongozi kuzingatia maadili ya ushirika ili kurejesha imani ya wakulima.
Kutokana na hali hiyo, TANECU imelazimika kuingilia kati katika baadhi ya maeneo na kuanza kulipa wakulima waliokuwa hawajapatiwa stahiki zao.
Akitoa mfano, Mwenyekiti wa chama hicho, Karim Chipola, amesema katika Chama cha Msingi cha Mihambwe kulibainika upotevu wa takriban shilingi milioni 149, huku hatua za kisheria dhidi ya waliohusika zikiendelea. Wakati huo huo, chama hicho kimeanza kulipa wakulima ili kupunguza athari walizokuwa wakizipata.
Baadhi ya wakulima waliohudhuria mkutano huo, akiwemo Said Nalola na Ally Mpini, wameonesha kuridhishwa na hatua ya chama kikuu kuingilia kati, wakieleza kuwa inaleta matumaini ya kulipwa fedha zao na kuimarika kwa usimamizi wa vyama vya msingi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!