Aliyekuwa Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameeleza namna alivyomfahamu marehemu William Vangimembe Lukuvi kisiasa akimtaja kama kiongozi wa kipekee aliyekuwa na uwezo wa kulinda maslahi ya chama chake bila kuvunja misingi ya uwajibikaji.
Katika andiko lake la heshima kumhusu Lukuvi, Zitto ameeleza kuwa Lukuvi hakuwa mwanasiasa wa kutumia vitisho, bali alikuwa mtu wa hoja, busara, na mwenye uwezo mkubwa wa kukubali matokeo hata pale alipozidiwa nguvu na upinzani bungeni.
“Alikuwa mwanasiasa katika maana halisi- si chombo tu cha madaraka ya dola. Alishindana kwa hoja, si kwa vitisho. Aliposhindwa, alikubali kushindwa kwa heshima na hakuweka kinyongo. Nje ya ukumbi wa bunge, alikuwa mchangamfu, mwenye ucheshi, na mwenye kuvutia- mwepesi wa kucheka, kutaniana, na kuahidi kuwa atakushinda wakati ujao”, ameeleza Zitto.
Zitto anakumbuka mwaka 2005, wakati Lukuvi alipokosa nafasi kwenye Baraza la Mawaziri na kuwekwa kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC). Katika kipindi hicho, Lukuvi alionesha msimamo mkubwa katika sakata la kampuni ya Alex Stewart, ambapo alishirikiana na wajumbe wengine kuhakikisha serikali inaacha kutumia kampuni hiyo na kuanza kukagua uzalishaji wa dhahabu yenyewe, jambo lililookoa mabilioni ya fedha.
“Katika vikao vile vikali vya PAC ndipo nilipoona tabia halisi ya Lukuvi: Mwanasiasa aliyeamini kwa dhati katika uwajibikaji, lakini aliyekataa kuruhusu jambo hilo kuharibu taswira ya chama chake. Alifanya kazi kwa hekima na kiasi- akihakikisha kuwa kamati haigeuzi suala hilo kuwa uwindaji wa kisiasa wa upande mmoja, huku akisisitiza kuwa ubadhirifu lazima ukomeshwe”, ameandika Zitto.
Baada ya kurejea kwenye nafasi ya Mnadhimu Mkuu wa Serikali mwaka 2010, Lukuvi alikumbana na changamoto mpya kutoka kwa kizazi cha vijana na wabunge machachari wa upinzani, akiongozwa na Tundu Lissu. Zitto anaeleza kuwa Lukuvi alipambana kuitetea serikali dhidi ya hoja nzito za Lissu, hata katika nyakati ngumu kama ripoti za CAG za 2012 na Operesheni Tokomeza.
Moja ya matukio yanayovutia zaidi ni wakati wa kashfa ya Tegeta Escrow. Zitto anasimulia kuwa usiku mmoja kabla ya kuwasilishwa kwa hoja hiyo bungeni, Lukuvi hakulala, akijaribu kutafuta mbinu walizopanga wapinzani lakini alishindwa.
“Usiku wa kuamkia siku ambayo hoja hiyo iliwasilishwa, Lukuvi hakulala. Alitembea katika viwanja vya Bunge hadi alfajiri, akijaribu kugundua mbinu yetu. Alishindwa. Asubuhi iliyofuata tulipokutana, alinitazama kwa tabasamu fupi na kusema: “Ninyi watoto wasumbufu, mmenishinda”, ameeleza Zitto.
Zitto amekiri kuwa mradi wa Julius Nyerere Hydropower (JNHPP) ndio ulikuwa mnyukano wao wa mwisho wa hoja. Wakati Zitto na wenzake walikuwa na hofu juu ya mradi huo, Lukuvi alisimama kidete kuutetea.
“Akiwa Waziri wa Ardhi chini ya Rais John Magufuli, Lukuvi alisimama imara kutetea mradi huo wakati wengi wetu tulielezea wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano na gharama zake. Katika mjadala ule, ilionekana kana kwamba nilimshinda. Lakini historia imethibitisha kinyume chake. Mradi ulikamilika. Sasa unazalisha umeme kwa ajili ya taifa letu. Hofu tulizozitoa hazijatokea. Laiti ningeweza kumpa mkono na kumwambia: Kaka, hili umenishinda”, amekumbusha Zitto.