Wajumbe wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wameshiriki katika semina ya Maadili ya Utumishi wa umma na kukumbushwa kuzingatia misingi na kanuni za maadili ya Utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao.
Wito huo umetolewa kwa watumishi hao na Bw. Hamad Bakari, Afisa Maadili Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais, Sekretariet ya Maadili ya Viongozi wa Umma wakati akitoa mada jana, tarehe 27 Machi, 2026 katika ukumbi wa Mikutano wa APC, jijini Dar es salaam.

Aidha viongozi hao wamekumbushwa kuzingatia matumizi sahihi ya taarifa; kuepuka vitendo vya rushwa au matumizi yoyote mabaya ya madaraka au wadhifa; kuepuka kutumia mali ya umma kwa maslahi binafsi na kulinda haiba wakati wa kazi na baada ya kustaafu.
Sambamba na hilo Bakari amesema, “mnapaswa kujali wateja wa nje na ndani, kuheshimiana na kuheshimu haki za faragha, lakini pia mnapaswa kutoa huduma kwa wakati.”

Bakari pia aliwakumbusha watumishi hao kujali muda wa kazi, kutoa huduma pasipo upenedeleo, kufanya kazi kwa ufanisi na kutokutoa taarifa kwa watu wasiohusika.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Ziwa, CPA Janet Nyoni akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Baraza walioshiriki katika semina hiyo amesema, “tutakwenda kuzingatia yale yote tuliyokumbushwa hapa katika kutimiza majukumu yetu ya kuhudumia umma kwa kuzingatia kanuni na taratibu za maadili ya utumishi wa Umma.”
