Latest Posts

ABDUL NONDO ATANGAZA NIA UBUNGE KIGOMA MJINI KUPITIA ACT WAZALENDO

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo Taifa, Abdul Omary Nondo, ametangaza rasmi nia ya kugombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025, kupitia chama hicho.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu ya kugombea kuteuliwa na chama chake kwa ajili ya uchaguzi huo siku ya Jumanne, Nondo amesema ametekeleza hatua hiyo kwa mujibu wa Ibara ya 21 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, pamoja na Ibara ya 11(c) ya Katiba ya ACT Wazalendo, toleo la mwaka 2024. Fomu hiyo imekabidhiwa kwake na Katibu wa ACT Jimbo la Kigoma Mjini, Iddi Adam Sumvya.

“Hii si mara yangu ya kwanza kuomba ridhaa ya chama kugombea ubunge wa Kigoma Mjini. Niliwahi kushiriki kura ya maoni mwaka 2020, ingawa kura hazikutosha na kiongozi wetu mstaafu Mh. Zitto Kabwe alipendekezwa kuwa mgombea,” amesema Nondo.

Amesema dhamira yake imebaki kuwa ileile ya kuwatumikia wananchi wa Kigoma Mjini na kwamba anaamini amekomaa kisiasa, ana uelewa wa changamoto za wananchi, na ana dhamira safi ya kuwa sehemu ya mabadiliko chanya.

Nondo pia amesisitiza kuwa endapo hatapita kwenye mchujo, ataendelea kushirikiana bega kwa bega na mgombea atakayeteuliwa kuhakikisha ushindi wa chama na kurejesha hadhi ya mji huo.

“Jimbo la Kigoma Mjini siyo jimbo la majaribio, siyo Jimbo la kuleta mizaha na kutafutia umaarufu. Ni Jimbo lenye wananchi waelevu wanaojua wanataka nini, na wanataka Mbunge wa namna gani, na ndiyo maana tumejizatiti kurejesha hadhi na heshima ya mji wetu wa Kigoma Mjini kwa kupiga kura, kulinda kura na kupambana dhidi ya hujuma zozote”, ameeleza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!