Latest Posts

ASK. GWAJIMA AENDELEA KUSIMAMIA MSIMAMO WAKE DHIDI YA UTEKAJI “SITAKI UTEKAJI TANZANIA”

Askofu Josephat Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe na Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, ametoa onyo kali dhidi ya vitendo vya utekaji vinavyodaiwa kushamiri nchini, akisisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakihusiki na utekaji, na kwamba mtu yeyote anayetekeleza vitendo hivyo anafanya kwa maslahi binafsi, si kwa niaba ya chama hicho.
 
Akizungumza Jumapili katika ibada ya kanisani kwake, wilayani Ubungo, Gwajima amesema licha ya kukosolewa na baadhi ya viongozi na wabunge wa CCM kwa kuzungumza hadharani kuhusu suala hilo, hatabadili msimamo wake dhidi ya utekaji, akisisitiza kuwa “utekaji si sera ya CCM.”
 
“CCM si chama cha watekaji. Mimi ni mwanachama wa CCM na sipingi chama changu, bali napinga utekaji. Hili nitalisimamia mpaka mwisho. Sitaki utekaji”, ameeleza Gwajima.
 
Kauli hiyo ya Gwajima imekuja baada ya kulaumiwa na baadhi ya viongozi na wabunge wa CCM kwa kuzungumza na wanahabari kuhusu utekaji na kupotea kwa watu nchini, huku akisisitiza kuwa hawezi kunyamaza wakati wananchi wanaendelea kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.
 
Gwajima amesema kuwa utekaji hauchagui mtu kwani umewakumba raia wa kawaida, viongozi wa dini na hata wanachama wa CCM. Alitoa mfano wa Sheikh Jabir Haidar Al Farsi wa Zanzibar, ambaye alikutwa amefariki dunia Mei 28, 2025 katika eneo la Bumbwisudi, baada ya kutoweka. “Baada tu ya kutoa tamko langu kuhusu utekaji, Sheikh Jabir alipatikana akiwa amekufa”, amesema Gwajima.
 
Aidha, ametaja tukio la kutoweka kwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoani Mwanza Daniel Chonchorio ambaye hajulikani alipo tangu Machi 23, 2025, akiongeza kuwa hali hiyo inapaswa kuishtua jamii nzima.
 
“Watekaji wanamteka mwanachama wa CCM, kiongozi wa dini, na mtu wa kawaida. Sasa ukinyamaza, hujui kama kesho wewe ndiye unafuata,” ameongeza.
 
Katika hotuba yake, Gwajima ameelezea kwa hisia kuwa ni muhimu jamii kuonyesha huruma kwa waliopotea na familia zao. Amesema: “Niliuliza, kama mwanangu Jordan angekutwa kama Mzee Kibao pale Tegeta, ameng’olewa macho na kuuawa, ningejisikiaje? Kwa nini hatuoni kilio cha wanyonge?”
 
Mbunge huyo aliweka wazi kuwa msimamo wake haupingani na CCM bali ni wa kusimamia utu, haki za binadamu na usalama wa raia. Amesisitiza kuwa yeyote anayempinga kwa hoja hiyo ana nia nyingine isiyolenga maslahi ya taifa.
 
Pamoja na sakata la Sheikh Jabir na mjumbe wa CCM Mwanza, Gwajima alitolea mfano tukio la kutekwa kwa mwanaharakati Mdude Nyagali, ambaye hajulikani alipo tangu Mei 2, 2025. Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya iliyotolewa Mei 10, 2025, uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
 
Gwajima amesema ataendelea kupaza sauti hadi pale ambapo vitendo vya utekaji vitakomeshwa nchini na haki kutendeka kwa wote waliopotea.
 
Mara kadhaa Jeshi la Polisi Tanzania limekuwa likitolea maelezo ya watu kutekwa na kuuawa. Mnamo tarehe 24 Agosti 2024, Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime alitoa onyo kwa watu kuacha tabia ambazo zinasababisha watu kudaiwa kupotea au kutekwa ambazo ni pamoja na wivu wa mapenzi, imani za kishirikina, tamaa za mali au fedha na kulipiza kisasi.
 
Aidha alitoa angalizo kwa baadhi ya watu wanaozungumzia matukio ya aina hii kutumia majukwaa yao kwa uangalifu ili kutoleta taharuki na kujenga uhasama.
 
Halikadhalika, alitoa rai kwa viongozi wa dini, wazee wa kimila, wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuona matatizo hayo yanayotokea ndani ya jamii, hivyo waendelee kujenga misingi bora ya kuyazuia kuanzia ngazi ya familia

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!