Katika kile kinachoonekana kama mabadiliko makubwa ya kisiasa, serikali ya mpito nchini Venezuela imeanza mchakato wa kuwaachilia huru wafungwa wanaotambulika kama wafungwa wa kisiasa na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu. Maafisa wa serikali wameitaja hatua hiyo kama “ishara ya nia njema” katika kipindi hiki cha mpito.
Hatua hii inakuja mara baada ya tukio la kushtua la kukamatwa kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro mjini Caracas na mamlaka za Marekani, ambapo anakabiliwa na tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya mjini New York. Marekani imekuwa ikishinikiza kuachiliwa kwa wafungwa hao kwa muda mrefu, ikilaani ukandamizaji uliofanywa wakati wa chaguzi na maandamano ya huko nyuma.
Miongoni mwa walionufaika na hatua hii ni raia watano wa Uhispania, huku duru za habari zikiashiria kuwa mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu, Rocio San Miguel, pia ameachiliwa.

Ingawa Jorge Rodriguez, Spika wa Bunge, alitangaza kuwa “idadi kubwa” ya watu watafunguliwa milango ya gereza, bado kuna mamia ya wafungwa wa kisiasa wanaoendelea kushikiliwa huku idadi kamili ya walioachiliwa ikisalia kuwa ndogo kwa sasa.