Umoja wa Afrika (AU) umeisimamisha nchi ya Guinea Bissau kushiriki katika shughuli zake zote, siku mbili baada ya jeshi kumpindua Rais Umaro Sissoco Embaló na kusitisha mchakato wa kutangaza matokeo ya uchaguzi yaliyotarajiwa kutolewa hivi karibuni.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, Mahmoud Ali Youssouf, alithibitisha kusimamishwa huko, akisema hatua hiyo inachukuliwa “mara moja” kufuatia ukiukaji wa misingi ya demokrasia katika taifa hilo dogo la Afrika Magharibi linalozungumza Kireno.
Mapinduzi hayo yalitangazwa Jumatano, ambapo jeshi lilisema limemuondoa madarakani Embaló na kuteua Jenerali Horta N’Tam- aliyekuwa Mkuu wa Majeshi kuwa Rais wa mpito kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Embaló, ambaye awali alikamatwa na wanajeshi, alifanikiwa kukimbilia Senegal siku ya Alhamisi.
Kwa upande mwingine, mgombea wa upinzani wa urais, Fernando Dias, anayesisitiza kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi, aliambia AFP kuwa yuko “salama” na anajificha ndani ya nchi.
Mapinduzi hayo yamekosolewa vikali kimataifa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alilaani hatua hiyo kama “ukiukaji usiokubalika wa misingi ya kidemokrasia”. Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) nayo imeisimamisha Guinea-Bissau kushiriki katika “vyombo vyake vyote vya kufanya maamuzi”.
Guinea-Bissau sasa inaungana na mataifa mengine yaliyowahi kusimamishwa na AU kutokana na mapinduzi, ikiwemo Mali, Burkina Faso, Niger, Sudan na hivi karibuni Madagascar. Hata hivyo, vikwazo dhidi ya Gabon iliyopinduliwa mwaka 2023 viliondolewa mwezi Aprili.