Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeanza rasmi mafunzo ya kuwajengea uelewa Maafisa Utamaduni na Maafisa Biashara wa Mikoa na Halmashauri kuhusu namna ya kusomana kwa mifumo ya AMIS (ya BASATA) na TAUSI (ya Serikali za Mitaa), ikiwa ni hatua muhimu ya kuondoa urasimu na kuboresha usimamizi wa shughuli za sanaa nchini.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa hivi karibuni kuhusu umuhimu wa kurasimisha sekta ya sanaa na kuboresha huduma kwa wasanii nchini.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti na Masoko BASATA, Mrisho Mrisho, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya kuwawezesha Maafisa Utamaduni na Maafisa Biashara kutambua kwa undani kazi mbalimbali za sanaa, ambazo awali zilikuwa hazieleweki vizuri katika ngazi ya Serikali za Mitaa.
“Tumekuja mara na kukutana na maafisa hawa ili kuwawezesha kuelewa mifumo hii na umuhimu wa urasimishaji katika sekta ya sanaa. Hii itarahisisha kazi kwa wasanii, vikundi vya sanaa, wamiliki wa kumbi na wadau wengine,” alisema Mrisho.
Kupitia mfumo wa AMIS, wasanii wataweza kujisajili na kupata vibali rasmi vya kufanya kazi zao, wakati mfumo wa TAUSI ukisaidia kurahisisha mawasiliano na usimamizi kutoka upande wa Serikali za Mitaa.
BASATA imesisitiza kuwa mafunzo hayo yanawawezesha maafisa wa halmashauri kuondoa urasimu na mianya ya rushwa, kwa kuwa sasa taarifa za wasanii na wamiliki wa miundombinu ya burudani zitakuwa wazi kwa pande zote kupitia mifumo hiyo ya kisasa.
Baadhi ya Maafisa Utamaduni waliohudhuria mafunzo hayo wamesema kuwa hatua hiyo ni mwarobaini wa changamoto nyingi zilizokuwa zikikumba sekta ya sanaa.
Hatua ya kusomana kwa mifumo ya AMIS na TAUSI ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha mazingira ya kazi kwa wasanii, kwa kuwapatia huduma bora, za haraka na zenye uwazi. Hii inajibu wito wa Rais Samia wa kufanya sanaa kuwa ajira rasmi na chanzo cha mapato kwa vijana.