Kiongozi wa chama cha National Unity Platform (NUP), Robert Sentamu Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, amejitosa tena katika kinyang’anyiro cha urais nchini Uganda, ambapo uchaguzi mkuu unatarajiwa kufanyika Januari 2026.
Kwa mujibu wa taarifa za chama hicho, siku ya Jumatatu viongozi waandamizi wa NUP akiwemo Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Joel Ssenyonyi, Katibu Mkuu wa chama, David Rubongoya pamoja na Msimamizi wa Hazina ya Kitaifa, Benjamin Katana, walichukua fomu ya kugombea urais kwa niaba ya Bobi Wine kutoka makao makuu ya Tume ya Uchaguzi.
Chama cha NUP kimetangaza kuwa kampeni zake zitaendeshwa chini ya kaulimbiu “Uganda Mpya Sasa”, ikilenga kuhamasisha ushiriki mkubwa wa wananchi katika upigaji kura.
“Uganda mpya tunayozungumzia ni nchi ambapo wananchi wote wanapata matibabu bora hospitalini, barabara zetu zinakuwa katika hali nzuri, na watoto wetu wanapata elimu bora katika shule zetu,” alisema Ssenyonyi akizungumza na vyombo vya habari baada ya kuchukua fomu.
Hii inakuwa mara ya pili kwa Bobi Wine kuwania nafasi ya urais dhidi ya Rais Yoweri Museveni, ambaye ameongoza taifa hilo kwa zaidi ya miongo mitatu. Katika uchaguzi wa mwaka 2021, Bobi Wine alimaliza katika nafasi ya pili baada ya kupata kura 3,475,398 sawa na asilimia 34.83 ya kura zote.