Rais wa Cameroon, Paul Biya, ambaye ana umri wa miaka 92 na anashikilia rekodi ya kuwa kiongozi mzee zaidi duniani anayeongoza nchi, ametangaza rasmi nia ya kugombea tena katika uchaguzi wa urais unaotarajiwa kufanyika Oktoba 12, 2025.
Kupitia taarifa fupi aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii leo, Biya alisema ameamua kugombea tena kufuatia “simu nyingi na za kusisitiza kutoka mikoa yote kumi ya nchi yetu na hata kutoka ughaibuni.”
“Mimi ni mgombea wa uchaguzi wa urais wa Oktoba 12. Uwe na uhakika kwamba azimio langu la kukuhudumia linalingana na changamoto kubwa zinazotukabili,” alisema Biya.
Rais huyo amekuwa madarakani tangu 1982 na hajawahi kushindwa katika uchaguzi wowote wa urais. Hii ina maana kuwa, iwapo atashinda tena, ataongoza taifa hilo la Afrika ya Kati hadi angalau mwaka 2032, na kufikisha takriban miaka 50 madarakani.
Hata hivyo, utawala wa Biya umekumbwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa makundi ya ndani na nje ya nchi, ukihusishwa na tuhuma za ufisadi, ukandamizaji wa haki za binadamu, na kushindwa kukabiliana na migogoro ya usalama, hasa katika maeneo ya kaskazini-magharibi na kusini-magharibi ya nchi hiyo.
Tangazo lake pia linakuja katika kipindi ambacho baadhi ya washirika wake wa muda mrefu kutoka mikoa ya kaskazini wametangaza kujitenga kisiasa, hatua inayoweza kutishia uungwaji mkono wake wa kisiasa.
Aidha, wito wa kimataifa na wa ndani umekuwa ukiongezeka, ukimtaka Biya kupisha kizazi kipya ili kuleta mwelekeo mpya wa uongozi.