



Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji katika sekta ya elimu ili kuongeza chachu kwa wanafunzi kujifunza masomo tofauti ikiwa ni pamoja na lugha mbalimbali zinazoambatana na ujuzi ili kurahisi upatikanaji wa ajira wanapomaliza masomo yao.
Amesema Serikali inawatia moyo wawekezaji binafsi kwenye elimu kuanzisha shule ili kuiunga mkono kwenye suala la utoaji elimu na haizuii anayetaka kuanzisha shule ya msingi na sekondari kwani ujuzi na maarifa ni kitu muhimu.
Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Kinondoni, Mtundi Nyamhanga aliyemuwakilisha Chalamila katika uzinduzi wa Mpango wa Mageuzi wa Shule ya Kimataifa ya Monti inayotumia Mtaala wa Kimataifa wa Cambridge.
Amesema mageuzi ya elimu yanayofanywa na shule hiyo ya Monti ni mfano wa kuigwa kutokana na elimu ya jumuishi — inayochanganya ubora wa kitaaluma, michezo, ubunifu na uvumbuzi inayotolewa na shule hiyo.
“Monti inawapa wanafunzi msingi imara wa kitaaluma huku ikikuza udadisi, fikra makini, na uelewa wa kidunia. Kupitia uwekezaji wake kwenye miundombinu ya michezo — kuanzia bwawa la kuogelea, uwanja wa mpira, hadi viwanja vya matumizi mchanganyiko — Monti inafundisha nidhamu, kazi za pamoja, na ustahimilivu kwa lengo la kuwandaa vijana siyo tu kushinda kwenye michezo, bali pia kushinda katika maisha.
“Mageuzi haya siyo tu ongezeko la idadi, bali ni mfano thabiti wa kile kinachoweza kufikiwa kupitia dhamira, uongozi dhabiti na kuamini katika elimu. Fatma, historia yako ni ukumbusho kuwa mambo makubwa huanza kwa hatua ndogo,” amesema.
Aidha, Mkuu wa shule na mwanzilishi wa shule hiyo ya kimataifa ya Monti, Fatma Fernandes amesema kama sehemu ya mageuzi hayo, shule hiyo itapanua huduma zake katika Kampasi ya Madale mwaka 2026 itakayoanza kutoa elimu ya sekondari.
“Hii ni hatua muhimu — kwani utaendeleza mpango wetu wa utoaji elimu kuanzia shule ya awali hadi sekondari, hapa hapa Dar es Salaam kwa kuzingatia mtaala wa Cambridge. Tunajenga si shule tu, bali urithi — urithi unaompa kila mtoto nafasi ya kustawi, kuongoza, na kuvutia,” amesema.
Amesema shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 150, mpango wake wa mageuzi unazingatia mambo makuu matatu ambayo ni elimu inayofuata mtaala wa Cambridge, ubora wa michezo, ubunifu na uvumbuzi.
Naye mmoja wa wazazi waliohudhuria uzinduzi huo, Thuwein Makamba amesema elimu inayotolewa katika shule hiyo ni ya kipekee hivyo anaamini elimu hiyo ni urithi tosha kwa mtoto.
“Wazazi wa sasa tunatakiwa kutambua kuwa, urithi kwa Watoto wetu ni elimu, wala sio majengo, mashamba na mali nyingine kwa sababu hizo zinaweza kuisha au kupotea, lakini elimu itakuwa urithi usiofutika,” amesema.