
Diwani wa Kata ya Ng’apa wilayani Lindi mkoani Lindi, Mhe. Issa Ngasha, amefanya mkutano maalum wa kuwashukuru wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kata hiyo kwa ushiriki wao katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, uliowezesha chama hicho kupata ushindi mkubwa katika nafasi za Udiwani, Ubunge na Urais.
Katika mkutano huo, Mhe. Ngasha ametoa misaada yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1.9 ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ustawi wa jamii na miundombinu ya chama.
Msaada huo umejumuisha mifuko arobaini (40) yenye vifaa muhimu vya kujifungulia kwa kina mama wajawazito, yenye thamani ya shilingi milioni moja, pamoja na tofali mia sita (600) zenye thamani ya shilingi laki tisa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya CCM Kata ya Ng’apa.
Akizungumza mbele ya wanachama na viongozi wa chama, Diwani huyo amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana katika uchaguzi huo yametokana na mshikamano na ushiriki wa wananchi, na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza umoja huo katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.
Sambamba na hayo, Mhe. Ngasha ameahidi kuendelea kushirikiana na wananchi, viongozi wa chama na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha huduma za kijamii na kiuchumi zinaboreshwa na miradi ya maendeleo inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi katika Kata ya Ng’apa.
Mkutano huo umehudhuriwa na wanachama wa CCM, viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama pamoja na wananchi wa kata hiyo.