Kampuni ya GN ECO SOLUTION COMPANY imewapiga msasa wafanyakazi wa Mpango wa Damu Salama ulio chini ya Wizara ya Afya kupitia mafunzo maalumu ya utimamu na ujenzi wa mshikamano kazini, mafunzo yaliyofanyika Februari 15, 2026 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wafanyakazi hao katika kuongeza ufanisi wa kazi, kuimarisha ushirikiano na kukuza umoja mahali pa kazi, sambamba na kuwahamasisha kufanya kazi kwa bidii katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Kupitia mbinu shirikishi na mazoezi mbalimbali ya vitendo, washiriki walipata fursa ya kujifunza namna bora ya kushirikiana katika kutatua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao, huku wakisisitizwa umuhimu wa kufanya kazi kama timu moja ili kufikia malengo ya taasisi.
Wawezeshaji kutoka GN ECO SOLUTION COMPANY waliongoza mafunzo hayo kwa weledi mkubwa, wakitoa maelekezo na motisha iliyolenga kuwajengea washiriki ari mpya ya kazi pamoja na kuwahamasisha kudumisha nidhamu, uwajibikaji na mawasiliano bora kazini.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, mwakilishi wa kampuni hiyo alisisitiza kuwa umoja na ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi ni nguzo muhimu katika kuongeza tija na kuboresha utoaji wa huduma kwa jamii. Aidha, alieleza kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za umma na binafsi katika kutoa mafunzo yenye tija yanayolenga kuimarisha rasilimali watu nchini.
Mafunzo hayo yamepokelewa kwa hamasa kubwa na washiriki, huku wakieleza kuwa yamewasaidia kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja, kuaminiana na kushirikiana katika kufanikisha majukumu yao kwa manufaa ya taasisi na jamii kwa ujumla.
