Latest Posts

IRAN YAIONYA MAREKANI: “TUKISHAMBULIWA, KAMBI ZENU MASHARIKI YA KATI ZITATEKETEA”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, ametoa onyo kali kwa Marekani kuwa nchi yake itajibu mashambulizi yoyote ya kijeshi kwa kupiga kambi za Marekani zilizopo Mashariki ya Kati, huku akisisitiza kuwa Iran ina haki ya kuendelea na urutubishaji wa madini ya Urani.
 
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha CBS cha Marekani, Jumapili, Araghchi amebainisha kuwa ingawa Iran haitaki vita, haitasita kulinda mamlaka yake. Alieleza kuwa kwa sababu makombora yao hayawezi kufika moja kwa moja kwenye ardhi ya Marekani, shabaha yao kuu itakuwa kambi za kijeshi za Marekani katika ukanda huo, kama ilivyotokea mwaka jana katika kambi ya Al-Udeid nchini Qatar.
 
Pamoja na lugha hiyo ya kijeshi, Araghchi ametoa matumaini ya kupatikana kwa suluhu ya kidiplomasia katika duru ijayo ya mazungumzo inayotarajiwa kufanyika mjini Geneva, Uswisi, Alhamisi ijayo.
 
“Ninaamini bado kuna nafasi nzuri ya kupata suluhu ya kidiplomasia ambayo inategemea mchezo wa pande zote kushinda (win-win). Tunafanya kazi katika vipengele vya mkataba na rasimu ya maandishi inakaribia kukamilika,” alisema Araghchi.
 
Changamoto kubwa katika mazungumzo hayo inabaki kuwa msimamo wa Iran kuhusu nishati ya nyuklia. Araghchi amesisitiza kuwa kama nchi huru, Iran ina haki ya kuamua yenyewe kuhusu urutubishaji wa Urani kwa matumizi ya kiraia, jambo ambalo Marekani imekuwa ikilipinga vikali kwa hofu ya kutengenezwa kwa silaha za nyuklia.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!