Rais wa Iran, Masoud Pezzekian, amesema kuwa vikosi vya kijeshi vya nchi yake viko tayari kwa hatua kali ikiwemo kushambulia ndani kabisa ya Israel, iwapo hali ya mvutano wa sasa itaendelea kuongezeka.
Akizungumza na televisheni ya Al Jazeera katika mahojiano maalum yaliyorushwa Jumanne, Pezzekian amesisitiza kuwa Iran haijafikia hatua ya kumaliza mpango wake wa nyuklia, bali teknolojia hiyo imo “akilini mwa wanasayansi wa Iran” na si katika “vituo vya nyuklia” kama inavyodaiwa na mataifa ya Magharibi.
“Israeli imetushambulia, nasi tumejibu kwa nguvu kubwa… lakini wao hawatangazi uharibifu walioupata,” amesema Rais Pezzekian, huku akisisitiza kuwa Iran ina haki ya kurutubisha madini ya uranium kwa matumizi ya amani.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Iran kushambulia kambi ya kijeshi ya Marekani ya Udeid nje kidogo ya mji wa Doha, Qatar. Hata hivyo, Pezzekian amesema Iran “haikuwa na nia ya kuishambulia Qatar” na kwamba tukio hilo lililenga ujumbe kwa Marekani na washirika wake kuhusu uwepo wa Iran katika ukanda huo.
Rais huyo pia amekiri kuwepo kwa changamoto za kiusalama katika jeshi la Iran, akitaja kuwa Israel imekuwa ikitumia “teknolojia ya hali ya juu kutoka Marekani” kuingilia mifumo ya ndani ya ulinzi wa Iran.
Mazungumzo hayo ni ya kwanza kwa Rais Pezzekian na chombo cha habari cha kimataifa tangu kuanza kwa mvutano wa kijeshi kati ya Iran, Marekani na Israel, ambao umesababisha hofu ya kuzuka kwa vita kamili ya kikanda.