Latest Posts

JESHI LA POLISI LAAHIDI KUENDELEA KUTOA HUDUMA BORA KWA JAMII

Jeshi la Polisi limesema litaendelea kutoa huduma bora kwa wateja wa ndani na nje ambao wanalitegemea Jeshi hilo huku likitoa wito kwa watendaji na watumishi wake kutambua maboresho makubwa yanayofanywa na Mkuu wa Jeshi Polisi nchini (IGP) Camilius Wambura, ambayo kimsingi yanaleta matokeo chanya kwa wananchi katika kuwapatia huduma bora.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa utawala na Menejimenti ya rasilimali watu wa Jeshi la Polisi CP Suzan Kaganda Juni 21, 2024 jijini Arusha wakati akifungua mafunzo yanayoendeshwa na mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) ambayo yamehusisha wakuu wa kikosi cha usalama Barabarani wilaya zote za kanda ya Kaskazini ambapo amewataka wakuu wa kikosi hicho baada ya kupatiwa mafunzo hayo kuonyesha mabadiliko katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

CP Kaganda ameongeza kuwa wakuu wa kikosi cha usalama Barabarani wanapaswa kuwasimamia na kuwapa maelekezo askari walio chini yao kuhusu namna bora ya kuongea na wananchi bila ya kutumia lugha ambazo si nzuri, huku akitumia jukwaa hilo kueleza kuwa lhivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa melekezo ya kuendelea kuboresha na kutoa huduma za kidigitali ili kuepusha masuala ya rushwa kwa askari wa usalama barabarani.

Aidha, CP Kaganda ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wakuu hao wa kikosi cha usalama Barabarani wilaya zote za kanda ya Kaskazini kuwa mwaka huu (2024) ni mwaka wa uchaguzi (uchaguzi wa serikali za mitaa) ambapo amewataka kujipanga vyema katika kusimamia usalama Barabarani ambazo wananchi watakuwa wakizitumia katika kushiriki zoezi la kampeni za uchaguzi utakao fanyika baadaye mwaka huu.

Naye, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Justine Masejo ametumia fursa ya mafunzo hayo kuwakaribisha katika mkoa huo ambao ni kitovu cha utalii hapa nchini na kuwaomba washiriki wa mafunzo hayo kutembelea vivutio vilivyopo mkoani humo.

Anselim Peter ambaye ni Mkurungenzi wa kitengo cha uendeshaji Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) amesema mfuko huo umekuwa na utaratibu wa kushirikiana na taasisi mbalimbali ambapo amebainisha kuwa awamu hiyo imelenga kutoa mafunzo kwa wakuu wa vikosi vya usalama Barabarani vya wilaya zote za kanda ya Kaskazini kuhusu namna ya kuchakata taarifa za ajali pindi zinapotokea na namna ya kudai fidia kwa waathirika wa ajali.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!